UN: Kubomoa turathi za kiutamaduni ni jinai ya kivita
Baaraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Ijumaa lilipitisha azimio la kihistoria kulinda turathi za kiutamaduni duniani dhidi ya makundi ya kigaidi wakati wa vita.
Azimio hilo litashughulikia masuala muhimu ya usafirishaji haramu wa bidhaa za kiutamaduni kama chanzo cha fedha za ufadhili wa ugaidi na pia linaweka bayana njia za kulinda turathi za kiutamaduni wakati wa vita ambako hali inakuwa tete. Akizungumzia kupitishwa kwa azimio hilo, mkurugenzi mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu UNODC, Yury Fedotov ,amesema bila ya shaka azimio hilo litaimarisha uwezo wa jumuiya ya kimataifa wa kushughulikia masuala hayo na pia ametoa mwito wa ushirikiano zaidi. Naye mkurugenzi mkuu wa Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO Bi Irina Bokova katika kikao hicho amesema utamaduni ndio kitambulisho cha mtu na ni muhimu ukalindwa.
Amesema uharibifu wa makusudi wa turathi za kiutamaduni ni uhalifu wa kivita na kuongeza kuwa kutetea na kulinda turathi za kiutamaduni ni zaidi ya suala la kiutamaduni, ni suala la usalama ambalo haliwezi kutenganishwa na lile la kutetea uhai wa binadamu. Hatua hiyo imekuja kufuatia uharibifu makubwa wa turathi za kiutamaduni ambao umekuwa ukifanywa na magaidi wakufurishaji hasa wa kundi la ISIS au Daesh huko Iraq na Syria. Magaidi hao mbali na ukatili na unyama wao dhidi wa wanadamu, pia wamekuwa wakibomoa turathi za staarabu za kale na zile za staarabu za Kiislamu na Kikristo huko Syria na Iraq.