Russia yatumia kura ya turufu kupinga azimio dhidi ya Syria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27706-russia_yatumia_kura_ya_turufu_kupinga_azimio_dhidi_ya_syria
Russia imetumia kura ya veto kupinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Syria, lililoandaliwa kwa tuhuma bandia kwamba serikali ya nchi hiyo ya Kiarabu imetimua silaha za kemikali dhidi ya raia katika eneo la Khan Sheikhoun.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 13, 2017 02:55 UTC
  • Russia yatumia kura ya turufu kupinga azimio dhidi ya Syria

Russia imetumia kura ya veto kupinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Syria, lililoandaliwa kwa tuhuma bandia kwamba serikali ya nchi hiyo ya Kiarabu imetimua silaha za kemikali dhidi ya raia katika eneo la Khan Sheikhoun.

Katika kikao cha jana cha Baraza la Usalama la UN, Russia ilitumia kura yake ya turufu kupinga rasimu ya azimio hilo dhidi ya Syria, iliyotayarishwa na Marekani, Uingereza na Ufaransa kwa madai yasiyo na msingi kuwa serikali ya Rais Bashar al-Assad iliua makumi ya raia katika mashambulizi yake ya silaha za kemikali.

Vladimir Safronkov, Naibu Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema lengo kuu la azimio hilo ni kuilaumu serikali ya Damascus kutokana na madai ambayo hadi sasa hayajafanyiwa uchunguzi huru na wa kina na wala hakuna mtu yeyote ametembelea eneo la tukio kutathmini hali ya mambo.

Mwanadiplomasia huyo wa Russia ameongeza kuwa, kulikubali azimio hilo ni sawa na kuhalalisha mashambulizi ya makombora ya Marekani dhidi ya Syria.

Russia akipiga kura ya hapana UNSC

Nchi kumi zilipiga kura ya ndio kuunga mkono azimio hilo, huku Bolivia na Russia zikipiga kura ya hapana. China, Ethiopia na Kazakhstan zilijizuia kulipigia kura azimio hilo.

Usiku wa kuamkia Ijumaa, Marekani ilivurumisha makombora 59  kutokea katika meli zake mbili za kivita katika bahari ya Mediterania na kukishambulia kituo cha jeshi la anga la Syria katika eneo la Shayrat katika mkoa wa Homs na kuua watu tisa wakiwemo watoto wanne na kujeruhi wengine kadhaa. 

Rais Donald Trump wa Marekai aliagiza kutekelezwa mashambulizi hayo, kwa kisingizio bandia kuwa serikali ya Syria iliua watu zaidi ya 80 kwa hujuma ya silaha za kemikali dhidi ya raia wa nchi hiyo, suala ambalo lilikanushwa vikali na Damascus.

Kombora la Tomahawk la US