WHO: Watu bilioni 2 duniani wanakunywa maji machafu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27708-who_watu_bilioni_2_duniani_wanakunywa_maji_machafu
Shirika la Afya Duniani limesema watu bilioni 2 kote duniani wanatumia maji machafu na kusisitiza kwamba kuna haja ya kufanyika juhudi za makusudi kuhakikisha kuwa kila mtu anapata maji safi ya kunywa na anaishi katika mazingira safi yenye mifumo ya kuondoa majitaka.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 13, 2017 07:28 UTC
  • WHO: Watu bilioni 2 duniani wanakunywa maji machafu

Shirika la Afya Duniani limesema watu bilioni 2 kote duniani wanatumia maji machafu na kusisitiza kwamba kuna haja ya kufanyika juhudi za makusudi kuhakikisha kuwa kila mtu anapata maji safi ya kunywa na anaishi katika mazingira safi yenye mifumo ya kuondoa majitaka.

Maria Neira, Mkuu wa Idara ya Afya ya Umma ya WHO amesema zaidi ya watu laki 5 wanapoteza maisha kila mwaka katika sehemu mbalimbali za dunia, kutokana na kunywa maji machafu na magonjwa yanayotokana na mazingira machafu.

Afisa huyo wa Shirika la Afya Duniani amefafanua kuwa: "Hii leo, watu bilioni 2 kote duniani wanakunywa maji machafu ambayo yana kinyesi, jambo ambalo linawaweka katika hatari ya kupatwa na magonjwa kama kipindupindu, ugonjwa wa kuhara damu, homa ya matumbo na ugonjwa wa kupooza (Polio).

Watu bilioni 2 duniani hawapati maji safi ya kunywa kama haya

Mwezi uliopita, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF ulitahadharisha kuwa, mtoto mmoja kati ya wanne ataishi katika eneo ambalo halina maji safi ya kunywa kufikia mwaka 2040.

Ripoti ya UNICEF iliyotolewa kwa mnasaba wa Siku ya Maji Duniani imeonyesha kuwa, watoto zaidi ya 800 wanapoteza maisha kila siku katika sehemu tofauti za dunia, kutokana na ugonjwa wa kuharisha, unaosababishwa na mazingira machafu na ukosefu wa maji safi ya kunywa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo mpya ya WHO, nchi nyingi hazitafikia Malengo ya Maendeleo ya Mileni MDGs yaliyopasishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2015, likiwemo suala la kuhakikisha watu wote wanafikiwa na maji safi ya kunywa na kuishi katika mazingira safi.