Kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu nchini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i28294-kuongezeka_chuki_dhidi_ya_uislamu_nchini_marekani
Matukio yanayohusiana na chuki dhidi ya dini Tukufu ya Uislamu yameongezeka kwa asilimia elfu moja nchini Marekani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 26, 2017 13:20 UTC
  • Kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu nchini Marekani

Matukio yanayohusiana na chuki dhidi ya dini Tukufu ya Uislamu yameongezeka kwa asilimia elfu moja nchini Marekani.

Gazeti la Independent limeandika kuwa baadhi ya matukio  na vitendo vya  chuki dhidi ya Uislamu huko Marekani ambavyo vimeripotiwa kufanywa na maafisa na wafanyakazi wa idara ya forodha na ile ya ulinzi wa mipaka ya nchi hiyo, vimeongezeka kwa karibu asilimia elfu moja katika wakati huu wa uongozi wa Rais Donald Trump huko Marekani. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, viwanja vya ndege vya kimataifa huko Marekani ambavyo viko chini ya idara ya forodha na ile ya ulinzi wa mipaka ya nchi hiyo ni maeneo makuu ambako panajiri vitendo vya kibaguzi na utumiaji mabavu dhidi ya wahajiri wa Kiislamu. Baraza la Uhusiano wa Kiislamu la Marekani pia limetangaza kuwa vitendo vya kibaguzi na udhihirishaji wa chuki dhidi ya Waislamu vilivyoripotiwa kufanywa na maafisa na wafanyakazi wa idara tajwa huko Marekani vimeongezeka sana katika muda wa miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu wa 2017. 

Wananchi wakiandamana Marekani kupinga marufuku  dhidi ya raia wa nchi sita za Kiislamu

Mkurugenzi wa Baraza la Uhusiano wa Kiislamu la Marekani anayehusika na udhibiti wa chuki dhidi ya Uislamu amesema kuwa amri ya Trump inayowapiga marufuku raia wa nchi za Kiislamu kuingia Marekani ina mahusiano ya moja kwa moja na kuongezeka vitendo vya kibaguzi na chuki dhidi ya Waislamu. 

Dikrii ya pili iliyotangazwa na Rais Donald Trump kuhusu wahajiri ambayo inawazuia raia wa nchi sita za Kiislamu kuingia Marekani, imepingwa na majaji wa majimbo kadhaa nchini humo.