Trump akariri msimamo wake dhidi ya mapatano ya nyuklia ya Iran
Rais Donald Trump wa Marekani amekariri msimamo wake wa huko nyuma dhidi ya mapatano ya nyuklia ya Iran yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji JCPOA.
Akizungumza Jumamosi kwa munasaba wa kuwadia siku 100 za utawala wake, Trump amedai kuwa mapatano ya nyuklia ya Iran na madola sita makubwa duniani yamekuwa na taathira hasi kwa uchumi wa Marekani.
Aidha ameendelea kudai kuwa, kufungamana na utekelezwaji mapatano ya nyuklia ya Iran ni jambo ambalo litakuwa na madhara kwa Marekani.
Trump amewahi kupinga mara kadhaa mapatano ya nyuklia ya Iran na kundi la 5+1 na kuyataja kuwa mapatano 'mabaya' na kwamba analenga kuyatizama upya. Hii ni katika hali ambayo Umoja wa Ulaya na nchi zingine zilizoshiriki katika mazungumzo ya nyuklia na Iran zinasisitiza kutekelezwa mapatano hayo.
Tarehe 14 Julai 2015, Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 ambazo ni Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Marekani na Ujerumani zilisaini mkataba kuhusiana na shughuli za nyuklia za Iran ambao utekelezaji wake ulianza Januari 16 mwaka uliopita wa 2016.
Hata hivyo Marekani, ambayo ni mmoja wa wanachama wa kundi la 5+1 inakwepa kutekeleza ahadi zake na badala yake imekuwa ikichukua hatua ambazo zinakiuka makubaliano hayo ya nyuklia.