Marekani yaihakikishia ushindi Israel katika mazungumzo na Waarabu
Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Rais wa Marekani ameuhakikishia ushindi utawala wa Kizayuni na kuutaka usiwe na wasiwasi kuhusu uungaji mkono wa Washington kwa Israel katika mazungumzo ya mapatano ya Mashariki ya Kati. Ikumbukwe kuwa Marekani ndiye mpatanishi katika mazungumzo ya utawala wa Kizayuni na Mamlaka ya Ndani ya Palestina.
Herbert Raymond McMaster, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Donald Trump ametembelea ubalozi wa utawala wa Kizayuni mjini Washington na kuutoa wasiwasi kuhusu uungaji mkono wa White House kwa Israel katika mazungumzo ya mapatano ya Mashariki ya Kati.
Afisa huyo mwandamizi wa Marekani katika masuala ya usalama ametembelea ubalozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel mjini Washington katika hali ambayo Jumatano, Donald Trump ameonana na Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina katika Ikulu ya White House.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imelaani mazungumzo hayo ya Mahmoud Abbas na Donald Trump na kusema hayana faida yoyote.
Mazungumzo ya mapatano baina ya utawala wa Kizayuni na Mamlaka ya Ndani ya Plestina yanasimamiwa na Marekani. Yalikwama kikamilifu mwezi Aprili 2014 baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kukanyaga makubaliano na ahadi zote za huko nyuma na kuendelea kupora ardhi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwenye ardhi hizo.