Umoja wa Mataifa wataka kusaidia wakimbizi wa Sudan Kusini
Umoja wa Mataifa umetaka wakimbizi wa Sudan Kusini wasaidiwe ili waweze kujikimu na matatizo mbalimbali wanayokabiliwa nayo.
Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR amesema kuwa, kunahitajika kiasi cha dola bilioni moja na milioni 400 ili kuwasaidia wakimbizi wa Sudan Kusini ambao wengi wao wapo katika hali mbaya kimaisha.
Filippo Grandi amesisitiza kuwa, ili kuwasaidia wakimbizi milioni moja na laki nane wa Sudan Kusini panahitajika kiasi cha dola bilioni moja na milioni 400.
Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR ametahadharisha kuwa, mapigano na machafuko mtawalia na kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu huko Sudan Kusini kumepelekea idadi kubwa ya watu kuyakimbia makazi yao.
Ripoti za Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR zinaonyesha kuwa, idadi ya wakimbizi wa Sudan Kusini imekuwa ikiongezeka kila siku.
Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.