UN yapasisha azimio la kuwarejesha nyumbani askari wake ‘wabakaji’
https://parstoday.ir/sw/news/world-i2914-un_yapasisha_azimio_la_kuwarejesha_nyumbani_askari_wake_wabakaji’
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio linalotaka kurejeshwa nyumbani kikosi cha kulinda amani cha umoja huo, ambacho askari wake wanatuhumiwa kuhusika na vitendo vya ubakaji.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 12, 2016 11:49 UTC
  • UN yapasisha azimio la kuwarejesha nyumbani askari wake ‘wabakaji’

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio linalotaka kurejeshwa nyumbani kikosi cha kulinda amani cha umoja huo, ambacho askari wake wanatuhumiwa kuhusika na vitendo vya ubakaji.

Azimio hilo limepasishwa kwa kura 14 kati ya 15 za nchi wanachama wa baraza hilo, huku Misri ikijizuia kupiga kura. Hilo ndilo azimio la kwanza kupasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa shabaha ya kukabiliana na madai ya ubakaji yanayowakabili wanajeshi wa kulinda amani wa umoja huo katika nchi mbali mbali duniani. Mwaka uliopita wa 2015, kuliripotiwa madai 69 ya ubakaji na kunajisiwa watoto wadogo na askari wa Umoja wa Mataifa katika nchi 10 tofauti duniani. Azimio hilo limepasishwa baada ya Ban Ki-Moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutoa wito wa kuchukuliwa hatua kali dhidi ya askari wa kulinda amani wa kimataifa waliohusishwa na vitendo vya kunajisi wanawake. Azimio hilo limepasishwa katika hali ambayo, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limedai kuwa binti wa miaka 12 amebakwa na askari wa UN katika Jamhuri ya Afrika ya Kati hivi karibuni. Askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wamekuwa wakikabiliwa na tuhuma nyingi za kubaka na kunajisi watoto wadogo.