UN: Watu milioni 1.3 wanahitaji misaada ya dharura Libya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i29406-un_watu_milioni_1.3_wanahitaji_misaada_ya_dharura_libya
Umoja wa Mataifa umesema watu zaidi ya milioni moja na laki tatu nchini Libya wanahitajia misaada ya dharura ya kibinadamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 21, 2017 23:40 UTC
  • UN: Watu milioni 1.3 wanahitaji misaada ya dharura Libya

Umoja wa Mataifa umesema watu zaidi ya milioni moja na laki tatu nchini Libya wanahitajia misaada ya dharura ya kibinadamu.

Filippo Grandi, Mkuu wa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amesema watu zaidi ya laki tatu wamelazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi wa ndani au nje ya nchi kutokana na mgogoro unaoendelea kushuhudiwa nchini humo.

Amesema shirika hilo linafanya kila liwezekanalo kushughulikia mgogoro wa kibinadamu unaoshuhudiwa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika akisisitiza kuwa wakimbizi wa ndani nchini humo hususan wanawake na watoto wadogo wapo katika hali mbaya ya kutamausha.

Nembo ya Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa

Kadhalika Mkuu wa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa amesema UNHCR inafuatilia kwa karibu ili kulipatia ufumbuzi wimbi la wahajiri wa Kiafrika kuelekea barani Ulaya kupitia Libya.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2017 hadi sasa zaidi ya wahajiri elfu 43 wameokolewa katika maji ya bahari ya Mediterranean huku wengine zaidi ya 1,150 wakihofiwa kufa maji baada ya boti walizokuwa wakitumia kusafiria kuzama.