Wahajiri 58 wafa maji bahari ya Mediterrania, 100 watoweka
https://parstoday.ir/sw/news/world-i29804-wahajiri_58_wafa_maji_bahari_ya_mediterrania_100_watoweka
Umoja wa Mataifa umesema wahajiri 58 aghalabu yao wakiwa ni watoto wadogo wamekufa maji katika Bahari ya Mediterrania karibu na pwani ya Libya wakijaribu kuingia barani Ulaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 30, 2017 11:03 UTC
  • Wahajiri 58 wafa maji bahari ya Mediterrania, 100 watoweka

Umoja wa Mataifa umesema wahajiri 58 aghalabu yao wakiwa ni watoto wadogo wamekufa maji katika Bahari ya Mediterrania karibu na pwani ya Libya wakijaribu kuingia barani Ulaya.

Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema mbali na vifo hivyo, hatima ya wahajiri wengine zaidi ya 100 haijulikani hadi sasa baada ya boti zao kuzama katika bahari hiyo wiki iliyopita.

Aidha taarifa hiyo iliyotolewa leo Jumanne na UNHCR imesema wahajiri wengine elfu kumi wameokolewa katika pwani ya Libya ndani ya siku nne wiki jana na kwa sasa wapo katika mji wa Pozzallo, kusini mwa Italia. 

Vifo hivyo vimepelekea idadi ya watu waliopoteza maisha mwaka huu wakivuka moja ya maeneo hatari zaidi baharini kwa lengo la kukimbia umasikini na vita barani Afrika na Mashariki ya Kati kupindukia 1,700.

Wahajiri wakiokolewa na Gadi ya Pwani ya Italia

Taarifa iliyotolewa na Gadi ya Pwani ya Libya inasema kwamba, tarehe 18 mwezi huu pekee wahajiri karibu elfu tatu waliokolewa katika maji ya nchi za Libya na Italia wakijaribu kuingia barani Ulaya.

Mwaka jana zaidi ya wahajiri 5,000 hususan wa Kiafrika walipoteza maisha kwa kuzama katika bahari ya Mediterania wakiwa katika safari hizo hatari za kuelekea Ulaya.