Malumbano ya Trump na vyombo vya mahakama vya Marekani
Katika hatua ambayo ni nadra kuwahi kushuhudiwa, Rais wa Marekani amemwamuru Waziri wa Sheria awashinikize majaji wa Mahakama Kuu ya Federali kuhusiana na kesi ya marufuku ya raia wa nchi kadhaa za Kiislamu kufanya safari nchini humo.
Huku kesi ya malalamiko dhidi ya amri za Rais wa Marekani za kupiga marufuku raia wa nchi kadhaa za Kiislamu kufanya safari nchini humo ikiendelea kusikilizwa kwenye Mahakama ya Federali, Trump ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa Wizara ya Sheria inapaswa iitake Mahakama ya Federali ichukue hatua za haraka za kuzuia raia wa nchi kadhaa za Waislamu kufanya safari nchini humo; hatua ambayo itadhamini usalama wa Marekani. Huku akieleza kwamba mahakama za nchi hiyo zinafanya kazi kisiasa na kwa mwendo wa kujikongoja, Trump ameongeza kuwa, kwa vyovyote vile serikali yake inafanya tathmini za uchunguzi wa kiwango cha juu kabisa kwa watu wanaokusudia kuingia Marekani ili kuhakikisha nchi hiyo inabaki salama.
Matamshi hayo na agizo hilo kwa Wizara ya Sheria linadhihirisha kuwa, matumaini ya White House ya kushinda kesi iliyoko hivi sasa kwenye vyombo vya juu kabisa vya mahakama na sheria vya Marekani yanazidi kupungua. Na hii ni katika hali ambayo, hatua ya Trump ya kumwongeza Neil Gorsuch kwenye jopo la majaji wa Mahakama Kuu ya Federali limeufanya mlingano wa kisiasa-kiidiolojia katika muundo wa mahakama hiyo uwe tena kwa manufaa ya wahafidhina. Hata hivyo kuwepo idadi kubwa zaidi ya majaji wahafidhina kulinganisha na waliberali kwenye mahakama za ngazi tofauti nchini Marekani ikiwemo mahakama za mwanzo, mahakama za rufaa na hatimaye Mahakama Kuu ya Federali hakuihakikishii ushindi serikali ya Donald Trump katika vita vyake na vyombo vya sheria vya nchi hiyo.
Hivi sasa amri za Trump za kupiga marufuku raia wa nchi kadhaa za Kiislamu kuingia Marekani limekuwa suala ambalo limeigusa kwa moja heshima na itibari ya kiongozi huyo. Wiki moja tu baada ya kuingia Ikulu ya White House, Trump alizua baa kwa kusaini sheria ya kutekelezwa papo kwa papo, iliyopiga marufuku raia wa nchi saba za Kiislamu ambazo ni Iran, Iraq, Syria, Yemen, Somalia, Sudan na Libya kuingia nchini humo. Kufuatia kizaazaa na hali ya tafrani iliyowapata raia wa Marekani wenye asili za nchi hizo katika viwanja vya ndege vya nchi hiyo, watu wenye kadi za kijani za ikama ya kuishi nchini humo pamoja na raia wa kigeni wenye viza halali za kuingia katika nchi hiyo, makundi mbalimbali ya kutetea haki za kiraia pamoja na mawakili na waendesha mashtaka wa majimbo ya Marekani walifungua mashtaka dhidi ya amri ya Trump; na kwa msaada wa majaji wakaweza kuzuia utekelezaji wake.
Kufuatia upinzani huo ambao ni nadra kuwahi kushuhudiwa dhidi ya dikrii ya Rais wa Marekani, Trump alisaini amri nyengine ambayo iliiondoa Iraq kwenye orodha ya nchi saba pamoja na kupunguza mbinyo kwa watu wenye kadi za kijani za ikama ya kuishi Marekani. Pamoja na hayo, mahakama zikatoa hukumu tena ya kusimamishwa utekelezaji wa amri hiyo mpya ya Trump, uamuzi ambao uliungwa mkono pia na mahakama ya rufaa.
Katika kukabiliana na uamuzi huo, Rais wa Marekani akaanza kutuma jumbe zenye maneno makali na ya hasira katika ukurasa wake wa Twitter akiwatishia wapinzani wake kukiona cha moto katika Mahakama Kuu ya Federali. Trump alikuwa na matumaini kuwa hatimaye chombo cha juu kabisa cha mahakama cha Marekani kitatoa hukumu kwa manufaa ya mpango dhidi ya wahajiri uliopitishwa na serikali yake. Tabán Mahakama Kuu ya Federali bado haijatoa uamuzi wake wa mwisho. Lakini pamoja na hayo inavyoonyesha, matarajio ya White House ya kutangazwa haraka uamuzi wa majaji wa Mahakama Kuu ya Shirikisho hayajathibiti; na pengine si ajabu hata mahakama hiyo pia ikatoa hukumu dhidi ya matakwa ya Trump.../