Mivutano na Trump yamfanya Mwanasheria Mkuu wa Marekani ajiuzulu
Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Sheria wa Marekani Jeff Sessions amejiuzulu kutokana na mivutano iliyojitokeza baina yake na Rais wa nchi hiyo Donald Trump.
Tovuti ya gazeti la Wall Street Journal imeandika kuwa, Jeff Sessions, Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Sheria wa Marekani amewasilisha barua yake ya kujiuzulu kufuatia mivutano iliyojitokeza kati yake na Rais wa nchi hiyo Donald Trump juu ya uchunguzi kuhusiana na uingiliaji wa Russia katika uchaguzi mkuu wa Marekani uliofanyika mwaka uliopita.
Duru moja ya kuaminika imetangaza kuwa imejitokeza mivutano mikali katika wiki za hivi karibuni baina ya Rais na Mwanasheria Mkuu wa Marekani baada ya Sessions kujivua na dhima ya kuchunguza kadhia ya Russia.
Kongresi ya Marekani inaendesha uchunguzi dhidi ya waziri huyo wa sheria ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo kuhusu mikutano na mazungumzo aliyofanya na balozi wa Russia mjini Washington.
Mbali na uchunguzi unaofanywa na bunge la Marekani kuhusiana na Jeff Sessions, Polisi ya Upelelezi ya nchi hiyo pia (FBI), inataka kuchunguza suala la mikutano aliyofanya waziri huyo wa sheria na balozi wa Russia.
Sessions amekanusha kufanya mazungumzo yoyote ya faragha na maafisa wa Russia.../