Theresa May ashindwa vibaya katika uchaguzi wa Uingereza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i30272-theresa_may_ashindwa_vibaya_katika_uchaguzi_wa_uingereza
Katika hali ambayo Theresa May Waziri Mkuu wa Uingereza ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Wahafidhina alikuwa anataraji kupata wingi mutlaki wa viti katika uchaguzi wa mapema wa bunge alioitisha nchini humo, chama chake hicho kimepata pigo kubwa na hata kupoteza wingi wa viti bungeni.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Jun 10, 2017 03:03 UTC
  • Theresa May ashindwa vibaya katika uchaguzi wa Uingereza

Katika hali ambayo Theresa May Waziri Mkuu wa Uingereza ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Wahafidhina alikuwa anataraji kupata wingi mutlaki wa viti katika uchaguzi wa mapema wa bunge alioitisha nchini humo, chama chake hicho kimepata pigo kubwa na hata kupoteza wingi wa viti bungeni.

Bi.May alikuwa na yakini kuwa chama chake kingepapa viti vingi zaidi kuliko kilivyokuwa navyo bungeni ili kwa njia hiyo serikali yake iweze kushiriki kwa nguvu katika mazungumzo ya kujiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit.

Matokeo ya uchaguzi wa bunge Uingereza yanaonyesha kuwa hakuna chama chochote kilichoweza kupata wingi mutlaki wa viti 326 vinavyotakiwa  katika bunge ili kuweza kuunda serikali. Chama cha May cha Wahafidhina au Conservatives kimepata viti 318 huku chama cha upinzani cha Leba kinachoongozwa na Jeremy Corbyn kikipata viti 262 na hivyo kuongeza idadi ya viti ikilinganishwa na bunge lililopita. Ni kwa msingi huo ndio wapinzani wakiongozwa na Corbyn wanamtaka May ajiuzulu lakini amekataa na kusema atasalia madarakani kwa ajili ya uthabiti na usalama wa nchi.  Baada ya kuonana na Malkia Elizabeth jana Ijumaa, Theresa May alisema ataunda serikali ya mseto na chama cha Democratic Union DUP cha eneo la Ireland Kaskazini.

Maudhui muhimu katika kampeni za uchaguzi wa Juni 8 Uingereza zilikuwa Brexit, usalama, mapambanao dhidi ya ugaidi, wakimbizi na ustawi wa kijamii.

Pamoja na hayo kuna sababu kadhaa ambazo zinatajwa kuchangia kushindwa vibaya May katika uchaguzi wa Alkhamisi.

Mchakato wa kujiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya tayari umeshaanza na Bi. May alikuwa na matumaini kuwa, iwapo angeshinda katika uchaguzi basi angekuwa na uwezo zaidi wa kuchukua misimamo mikali katika mazungumzo ya kujiondoa nchi hiyo kwenye umoja huo ambayo yamepangwa kuanza tarehe 19 mwezi huu wa Juni. Lakini matokeo haya ya uchaguzi yanaonyesha kuwa  wananchi wengi wa Uingereza hawajaridhishwa na sera pamoja na misiamamo ya serikali ya May kuhusu kujiondoa katika Umoja wa Ulaya.

Wataalamu wa mambo wanasema kujiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya kutakuwa na taathira mbaya za kiuchumi katika nchi hiyo na hivyo kuna hitilafu za kimsingi baina ya wanasiasa kuhusu namna ya kusimamia mchakato huo wa Brexit. Kati ya masuala muhimu ni namna Uingereza itakavyoweza kushiriki katika soko la pamoja la Ulaya na pia suala la usafiri huru baina ya raia wa Ulaya na Uingereza. Katika hali ambayo chama cha Wahafidhina kinasema chaguo bora zaidi ni kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, chama cha Leba kinasema lengo lake ni kujiondoa katika umoja huo sambamba na kuhakikisha Uingereza inanufaika na soko la pamoja la Ulaya huku haki za raia wa Uingereza zikilindwa katika umoja huo.

Hakuna shaka kuwa Uingereza ikiondoka rasmi katika Umoja wa Ulaya pasina kufikia mapatano kuhusu uwezo wake wa kushiriki katika soko la pamoja jambo hilo litapelekea kuongezeka gharama za kufanya biashara baina ya Umoja wa Ulaya na  Uingereza.

Mapambano dhidi ya ugaidi ni nukta nyingine iliyoibua mjadala mkali katika kampeni za uchaguzi nchini Uingereza.

Majeruhi katika hujuma ya kigaidi ya eneo la London Bridge hivi karibuni

Kiongozi wa chama cha Leba Jeremy Corbyn akizungumza baada ya hujuma za kigaidi hivi karibuni nchini Uingereza alikosoa vikali serikali ya Wahafidhina na kusema imeshindwa kusimamia usalama kwa kupunguza idadi ya maafisa wa polisi. Aidha alisema moja ya sababu za hujuma za kigaidi ni kuwa Uingereza inajiingiza katika vita katika maeneo mengine duniani. Ukosefu wa Usalama Uingereza ni jambo ambalo limepelekea raia wengi wa nchi hiyo watake mabadiliko katika sera za kigeni ili kuzuia hujuma za kigaidi.

Kwa vyovyote vile, matokeo ya uchaguzi Uingereza yanatathminiwa kuwa ni kufeli kwa Waziri Mkuu Theresa May hata kama chama chake kimepata wingi wa viti katika uchaguzi huo. May alicheza kamari kubwa ya kisiasa kwa kuitisha uchaguzi wa mapema kwa sababu yeye na wapambe  wake walikuwa na yakini ya kupata ushindi wa kishindo lakini sasa si tu kuwa idadi ya viti vya chama chake vimepungua bali pia analazimika kuunda serikali ya mseto na chama ambacho hakina umashuhuri. Kwa msingi huo May atakuwa na wakati mgumu sana katika mazungumzo ya Brexit. Matokeo ya uchaguzi Uingereza hayajapelekea tu kudhofika May na hata kuwepo uwezekano wa kumlazimu ajiuzulu bali pia ni ishara kuwa waliowengi nchini Uingereza, hasa vijana, hawaridhishwi na hali ya sasa ya kisiasa nchini humo.