Waislamu wazidi kunyanyaswa nchini Uingereza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i30630-waislamu_wazidi_kunyanyaswa_nchini_uingereza
Vitendo vya unyanyasaji dhidi ya Waislamu vimeongezeka nchini Uingereza hasa baada ya kutokea mashambulizi ya kigaidi katika miji ya Manchester na London.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jun 18, 2017 03:23 UTC
  • Waislamu wazidi kunyanyaswa nchini Uingereza

Vitendo vya unyanyasaji dhidi ya Waislamu vimeongezeka nchini Uingereza hasa baada ya kutokea mashambulizi ya kigaidi katika miji ya Manchester na London.

Gazeti la al Quds al Arabi linalochapishwa mjini London limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, licha ya Waislamu wa Uingereza kulaani vikali mashambulizi hayo ya kigaidi na kusisitiza kwamba vitendo hivyo ni kwa madhara ya jamii ya Uingereza wakiwemo Waislamu, lakini pamoja na hayo, unyanyasaji dhidi ya Waislamu umeongezeka.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi za Manispaa ya London, vitendo vya unyanyasaji dhidi ya Waislamu vimenogezeka mara tano tangu yalipotokea mashambulio ya kigaidi mjini humo.

Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa Uingereza, Mohammad Kozbar

 

Naye Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa Uingereza Mohammad Kozbar, ameliambia gazeti la al Quds al Arabi kwamba, inasikitisha kuona kuwa Waislamu ndio wanaolipiziwa kisasi cha mashambulio ya kigaidi licha ya kwamba wanapinga vikali mashambulizi hayo.

Amesema, kuvunjiwa heshima misikiti, kutumiwa Waislamu ujumbe wa vitisho na wa kulipiza kisasi kwenye mitandao ya kijamii n.k, ni miongoni mwa unyanyasaji wanaofanyiwa waziwazi Waislamu.

Amesema, hayo yote yanatokana na ujinga uliotanda katika jamii ya Uingereza kuhusiana na dini tukufu ya Kiislamu, hivyo kuna wajibu wa kufanyika jitihada kubwa zaidi za kuonyesha sura halisi ya Uislamu na kupinga kikamilifu vitendo vyote vya kigaidi vinavyohusishwa na dini hiyo ya Mwenyezi Mungu.