Waziri wa zamani wa Lebanon, mjumbe mpya wa UN nchini Libya
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limemuidhinisha Ghassan Salame, raia wa Lebanon kuwa mjumbe maalumu wa umoja huo katika masuala ya Libya.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeafiki kuteuliwa Salame waziri wa zamani wa utamaduni nchini Lebanon kuchukua sehemu ya Martin Kobler kama mjumbe maalumu wa umoja huo Libya.
Tokea Oktoba mwaka 2011 baada ya kuuawa dikteta wa miaka 40 wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi, Libya ilitumbukia katika machafuko na mgogoro wa kisiasa. Umoja wa Mataifa umekuwa na nafasi muhimu katika masuala ya Libya kabla na baada ya kuangushwa utawala wa Gaddafi.
Tokea vianze vita vya ndani Libya, Umoja wa Mataifa umepitisha maazimio mawili, nambari 1970 na 1973 sambamba na kutoa idhini ya kutumwa vikosi vya kulinda amani vya kimataifa nchini humo.
Umoja huo pia baada ya kifo cha Gaddafi umekuwa na mjumbe maalumu katika masuala ya Libya kwa lengo la kusaidia katika mchakato wa kurejesha utulivu na kuundwa serikali mpya ili kuhitimisha mgogoro katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.
Mwakilishi wa kwanza wa Umoja wa Mataifa Libya alikuwa Bernardino Leon, raia wa Uhispania. Lengo kuu la Leon lilikuwa ni kuhitimisha mapiganao makali yaliyokuwa yakitokota nchini humo ili kuwezesha kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa. Lakini alimuachia Martin Kobler wa Ujerumani nafasi yake hiyo pasina kufikia malengo yake bali hata Libya tayari ilikuwa na serikali mbili hasimu.
Martin Kobler naye kuanzia Novemba mwaka 2014 alichukua wadhifa wa mjumbe maalumu na sasa baada ya miezi 31 anaiacha nafasi hiyo inayochukuliwa na Ghassan Salame wa Lebanon.
Moja ya mafanikio makubwa zaidi ya Kobler ni kufikiwa Mapatano ya Skhirat lakini baada ya kupita miezi 18 tangu kufikiwa mapatano hayo, siku tu kuwa hayajatekelezwa bali Libya sasa inashuhudia kuwepo serikali tatu hasimu. Moja iko mjini Tobruk, ya pili iko katika mji mkuu Tripoli na ya tatu inajulikana kama Serikali ya Umoja wa Kitaifa chini ya uongozi wa Faiz Siraj.
Kwa hivyo tunapaswa kusema kuwa Ghassan Salame anachukua nafasi yake kama mjumbe wa tatu maalumu wa Umoja wa Mataifa Libya, katika hali ambayo umoja huo umeshindwa katika jitihada zake za kuunda serikali ya umoja wa taifa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Nukta nyingine ni kuwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anamteua Salame kuwa mjumbe wake mpya Libya katika hali ambayo awali nafasi hiyo ilikuwa imepangwa ichukuliwe na Mpalestina Salam Fayyaz, lakini uteuzi huo ukapingwa vikali na Nikki Haley balozi wa kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ambaye alidai kuwa umoja huo ulikuwa unapinga muitifaki wa Washington na kuipendelea Palestina.
Hivi sasa tunapaswa kuona iwapo Salame ambaye ni Mwarabu Mlebanoni ataweza kufanikiwa baada ya Leone Mhispania na Kobler Mjerumani kushindwa kufikia malengo waliokusudia Libya, hasa ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa.