Watu 140 wafukiwa katika maporomoko ya udongo China
https://parstoday.ir/sw/news/world-i30908-watu_140_wafukiwa_katika_maporomoko_ya_udongo_china
Serikali ya China imetangaza habari ya kufukiwa watu 140 katika maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kali katika maeneo ya kusini magharibi mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 24, 2017 09:47 UTC
  • Watu 140 wafukiwa katika maporomoko ya udongo China

Serikali ya China imetangaza habari ya kufukiwa watu 140 katika maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kali katika maeneo ya kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Taarifa iliyotangazwa leo na China imesema kuwa, maporomoko ya ardhi yametokea katika mkoa wa Sichuan ambapo jumla ya nyumba 40 ambazo walikuwa wanaishi ndani yake watu 140 zimefukiwa na udongo. Kwa mujibu wa habari hiyo, wafanyakazi wa kutoa misaada wametumwa kwenda eneo hilo na kuanza kutafuta miili ya wahanga wa ajali hiyo.

Mandhari ya maporomoko hayo

Siku chache zilizopita, mamlaka ya hali ya hewa kwa kushirikiana na idara ya kukabiliana na mafuriko na majanga ya kimaumbile nchini China sambamba na kuonya juu ya hali hiyo, zilitangaza kuwepo uwezekano wa kunyesha mvua kali katika maeneo tofauti ya nchi hiyo yakiwamo ya kusini magharibi. Aidha mvua ambazo zimekuwa zikinyesha katika miezi ya Mei, Juni na Julai zimekuwa zikisababisha hasara kubwa za mali na roho hususan katika maeneo ya kusini mwa nchi.

Shughuli ya uokoaji ikiendelea katika eneo la tukio

Janga kubwa zaidi la kimaumbile lililowahi kuikumba nchi hiyo ya Asia, ni mafuriko yaliyotokea maeneo ya kusini mwa nchi hiyo hapo mwaka 1998 ambapo karibu watu 4000 walipoteza maisha.