Buriani dola la "khilafa" bandia la Daesh
https://parstoday.ir/sw/news/world-i31154-buriani_dola_la_khilafa_bandia_la_daesh
Televisheni ya taifa ya Iraq jana ilitangaza rasmi habari ya kukomeshwa na kuangamizwa kundi la Daesh katika mji wa Mosul nchini humo. Habari hiyo iliyokosha na kufurahisha nyoyo za Wairaq na watu wengi wapenda haki na uadilifu kote duniani ilikuwa hitimisho la dola bandia la khilafa ya mawahabi la Daesh ambalo lilianzishwa Juni 2014 kwa ushirikiano wa chama cha Baathi kilichovunjwa huko Iraq, kwa msaada wa Saudi Arabia na washirika wake.
(last modified 2026-01-14T11:42:18+00:00 )
Jun 30, 2017 08:51 UTC
  • Buriani dola la

Televisheni ya taifa ya Iraq jana ilitangaza rasmi habari ya kukomeshwa na kuangamizwa kundi la Daesh katika mji wa Mosul nchini humo. Habari hiyo iliyokosha na kufurahisha nyoyo za Wairaq na watu wengi wapenda haki na uadilifu kote duniani ilikuwa hitimisho la dola bandia la khilafa ya mawahabi la Daesh ambalo lilianzishwa Juni 2014 kwa ushirikiano wa chama cha Baathi kilichovunjwa huko Iraq, kwa msaada wa Saudi Arabia na washirika wake.

Baada ya jeshi la Iraq kukomboa Msikiti Mkuu wa al Nuri huko magharibi mwa Mosul, Wizara ya Ulinzi ya Iraq ilitangaza kuwa: Ardhi yote ya Mosul imekombolewa kutoka kwenye makucha ya Daesh. Kamanda wa Operesheni ya Ukombozi wa Mosul, Meja Jenerali Abdul Amir Rashiid Yarallah amesema: Kikosi cha kupambana na ugaidi cha Iraq jana Alkhamisi kilifanikiwa kudhibiti kikamilifu msikiti ulioharibiwa na Daesh wa al Nuri. Msikiti huo uliharibiwa na kulipuliwa kwa mabomu na wapiganaji wa Daesh wakati jeshi na wapiganaji wa makundi ya kujitolea ya Iraq yalipokuwa yanasonga mbele kuelekea katikati ya mji huo. Kushindwa kwa Daesh na kukombolewa Msikiti wa al Nuri uliokuwa na umri wa miaka 850, ni ushindi mkubwa na wa kihistoria wa jeshi la Iraq na washirika wake. Msemaji wa jeshi la Iraq, Jenerali Yahya Rasul amesema: Kukombolewa Msikiti wa al Nuri kumehitimisha dola bandia la Daesh katika adhi ya Iraq.

Mwezi Juni mwaka 2014 wakati kundi la kigaidi la Daesh lilipotwaa udhibiti wa mji wa Mosul, kiongozi wa kundi hilo, Abu Bakr al Baghdadi alielekea kwenye msikiti huo na kutangaza dola la "khilafa" katika hotuba aliyoitoa ndani ya msikiti huo. Hivyo Msikiti wa al Nuri ulikuwa nembo ya nguvu kwa kundi hilo na ulikuwa na umuhimu mkubwa katika sera na siasa zake. Pamoja na hayo inatupasa kukumbusha kwamba, kuangamizwa utawala wa Daesh nchini Iraq hakuna maana ya kukombolewa kikamilifu vitongoji vyote vya maeneo ya kale ya mji wa Mosul. Hata hivyo suala hilo lina maana kwamba, Daesh kama kundi nchini Iraq imebakia katika historia na inakadiriwa kuwa, wapiganaji chini ya 200 waliosalia wa kundi hilo wanazingirwa na jeshi la Iraq katika maeneo kadhaa ya kale ya mji wa Mosul.  

Ushindi wa jeshi na wapiganaji wa makundi ya kujitolea nchini Iraq dhidi ya mawahabi na matakfiri wa Daesh ni matokeo ya idara na azma yao ya kweli na wamefanikiwa kung'oa mzizi wa kundi hilo habithi katika kipindi cha miezi tisa tu baada ya kulikalia kwa mabavu eneo kubwa la Iraq na kueneza ufisadi na uharibifu mkubwa wa watu na vitu kwa kipindi cha miaka 3.

Kundi la Daesh likimchoma moto raia

Katika uwanja huu inatupasa kupongeza mchango wa viongozi wakuu wa dini nchini Iraq katika kufanikisha mapambano ya kuangamiza kundi la kiwahabi na dola la khilafa bandia la Daesh. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, fatwa iliyotolewa na Ayatullah Ali Sistani, kiongozi mkuu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq, ilizidisha mshikamano, umoja na azma ya jeshi la nchi hiyo na makundi ya kujitolea ya wananchi ya kulimaliza kabisa kundi hilo la kiwahabi. Vilevile tunatoa pongezi makhsusi kwa makundi ya kujitolea ya wananchi ya al Hash'du Shaabi ambayo ni miongoni mwa sababu kuu za kupatikana ushindi huo mkubwa na wa kihistoria kwa Wairaq na Waislamu kwa ujumla. Taathira ya makundi hayo ya wananchi yaliyoingia kwenye medani ya vita kutii amri na fatwa za viongozi wa kidini, ilikuwa kubwa kiasi kwamba, zilifanyika njama na jitihada kubwa ndani na nje ya Iraq za kutaka kuyazima makundi hayo na kuyazuia kupambana na kundi la Daesh. Hata hivyo serikali na wananchi wa Iraq hawakusalimu amri mbele ya mashinikizo na njama hizo na walisisitiza zaidi juu ya umuhimu wa makundi hayo ya wananchi katika vita na mapigano ya kuliangamzia kundi hilo la Daesh. Umuhimu wa makundi hayo ya kujitolea ya wananchi unadhihiri vyema zaidi hii leo baada ya kuporomoka dola la khilafa bandia la Daesh.

Makundi ya kujitolea ya al Hashd al Shaabi

Kuangamizwa kile kinachoitwa "khilafa" na dola bandia la Daesh huko Mosul kumethibitisha tena kwamba, umoja na mshikamano ndiyo wenzo bora na upanga wenye makali zaidi wa kupambana na ugaidi. Vilevile mafanikio na ushindi wa kihistoria wa Wairaq huko Mosul si ushindi wa upande mmoja tu, bali hii leo mbali na taifa la Iraq mataifa mengine duniani hususan yale yaliyodhurika na kuathiriwa na ugaidi wa Daesh na mawahabi wa kitakfiri pia yanasherehekea ushindi na mafanikio hayo.

Shari ya mawahabi na makatili wa kundi la Daesh imekatwa kichwa kwa sasa nchini Iraq, lakini inatupasa kukumbuka kuwa, balaa na shari ya kundi hilo la kigaidi bado inawatesa na kuwaumiza wanadamu katika maeneo mengine ya dunia. Hivyo, mafanikio ya Wairaq yanapaswa kuwa kigezo chema cha kuigwa katika mapambano dhidi ya ugaidi hususan kwa madola yanayojinadi na kudai kupambana na ugaidi kwa maneno na kaulimbiu zisizoambatana na matendo na azma ya kweli.