Zaidi ya watu 100 wahofiwa kuaga dunia katika zilzala nchini China
https://parstoday.ir/sw/news/world-i32902-zaidi_ya_watu_100_wahofiwa_kuaga_dunia_katika_zilzala_nchini_china
Serikali ya China imetangaza kuwa ina wasi wasi watu zaidi ya 100 wamepoteza maisha yao katika mkasa wa mtetemeko wa ardhi ulioukumba mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa nchi hiyo ya Asia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 09, 2017 02:48 UTC
  • Zaidi ya watu 100 wahofiwa kuaga dunia katika zilzala nchini China

Serikali ya China imetangaza kuwa ina wasi wasi watu zaidi ya 100 wamepoteza maisha yao katika mkasa wa mtetemeko wa ardhi ulioukumba mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa nchi hiyo ya Asia.

Duru za habari zinasema watu 13 wamefariki dunia na wengine karibu 180 wamepata majeraha katika zilzala ya kwanza yenye ukubwa wa 7 kwa kipimo cha Rishta katika mji wa Guangyuan mkoani hapo.

Shirika la habari la Xinhua limeripoti kuwa, watalii 6 ni miongoni mwa watu walioaga dunia katika mkasa huo na kwamba wengine 31 elfu wamehamishwa na kupelekwa katika maeneo salama.

Sehemu ya madhara ya zilzala huko Sichuan, China

 

Gazeti la People's Daily la China limeripoti kuwa, watu 32 wameaga dunia katika mtetemeko mwingine wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 6.6 kwa kipimo cha Rishta uliotokea katika eneo la Xinjiang, umbali wa kilomita elfu mbili kutoka eneo la zilzala ya kwanza.

Mkoa wa Sichuan wa kusini magharibi mwa China umekuwa ukikumbwa na mitetemeko ya ardhi mara kwa mara.

Zilzala kubwa iliyowahi kushuhudiwa katika eneo hilo katika miaka ya hivi karibuni ni ile ya mwaka 2008, ambapo watu 70 elfu walipoteza maisha.