UN yataka kufanyike uchunguzi kuhusu mgogoro wa Myanmar
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limetaka kupewa uwezo kamili wa kuchunguza mgogoro wa sasa wa Myanmar bila ya mpaka wala kizuizi.
Baraza hilo limetangaza leo kwamba, kuna umuhimu mkubwa kwa wawakilishi wa Umoja wa Mataifa kukagua moja kwa moja maeneo ya Myanmar yanayokumbwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na maafa ya kutisha.
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limeongeza kuwa, mgogoro wa kibinadamu katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar unapaswa kupewa mazingatio makubwa haraka iwezekanavyo.
Jana Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alimkosoa vikali Aung San Suu Kyi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Myanmar na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel na kumtaka kuchukua hatua za haraka kukomesha mateso na mauaji yanayofanywa dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa Myanmar.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, Aung Suu Kyi na serikali ya Myanmar wanapaswa kukomesha mara moja operesheni za jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa Rohingya.
Maelfu ya Waislamu wa Rohingya wameuawa na malaki ya wengine kulazimishwa kukimbia makazi na nchi yao kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Mabudha wakishirikiana na jeshi la serikali ya Myanmar.