Putin na Salman wakutana kwa mazungumzo ya faragha mjini Moscow
Mfalme Salman bin Abduaziz wa Saudi Arabia jana alikutana na Rais Vladimir Putin wa Russia katika ikulu ya Kremlin mjini Moscow.
Pande mbili hizo zilikuwa na mazungumzo ya faragha yaliyojadili masuala ya nchi mbili na ya kieneo. Mazungumzo ya Rais wa Russia na Mfalme wa Saudia yalihudhuriwa pia na maafisa kadhaa wa nchi mbili hizo.
Akizungumza baada ya mkutano huo, Rais Putin alisema kuwa wamekuwa na mazungumzo mazuri ya kina kwa njia ya faragha juu ya uhusiano wa pande mbili na hali ya mambo katika eneo la Mashariki ya Kati.

Mfalme wa Saudi Arabia juzi aliwasili Russia akiambatana na ujumbe wa nchi yake kwa ajili ya ziara ya siku nne nchini humo. Ukiwa mjini Moscow, ujumbe wa Saudi Arabia umeripotiwa kusaini hati za makubaliano ya ushirikiano zaidi ya 15 huku nchi hiyo ikifunga mikataba ya mabilioni ya dola na Russia katika sekta ya nishati na masuala ya kijeshi.
Mbali na mikabata hiyo iliyosainiwa, Moscow imekubali kuiuzia Riyadh mfumo wa kisasa wa makombora aina ya S-400.