Bangladesh kufunga uzazi wakimbizi Waislamu Warohingya kutoka Myanmar
Maafisa wa afya nchini Bangladesh wamesema wameanzisha mpango maalumu wa kupunguza idadi ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya ambao wamekimbia mauaji ya kimbari huko Myanmar na kujazana katika kambi za wakimbizi nchini Bangladesh.
Maafisa wa kupanga uzazi wametoa wito kwa serikali ya Bangladesh kuidhinisha mpango wa kufunga uzazi wa wanawake na wanaume wanaoishi katika kambi zenye idadi kubwa ya watu katika wilaya ya Cox's Bazar ambayo inapakana na wilaya ya Rakhine ya Myanmar ambayo imeshuhudia mauaji ya kimbari ya Waislamu.
Wanawake wengi Waislamu Warohingya wamekuwa wakipata mimba za haraka kwa imani kuwa hiyo ndio njia pekee ya kuepuka kunajisiwa na wanajeshi wa Myanmar au wahalifu katika kambi za wakimbizi. Wakuu wa Bangladesh wanasema, wanawake 20,000 Warohingya hivi sasa wana mimba na wengine 600 wamejifungua baada ya kuwasili katika kambi za wakimbizi.
Pintu Kanti Bhattacharjee mkuu wa huduma za kupanga uzazi katika wilaya hiyo ya mpakani amesema kufunga uzazi ndio njia bora zaidi ya kudhibiti ongezeo la kasi la idadi ya wakimbizi eneo hilo.
Inaaminika kuwa wakimbizi zaidi ya laki sita wamevuka mpaka na kuingia Bangladesh kutoka Myanmar tokea Agosti 25 wakati wimbi jipya la mauaji dhidi ya Waislamu lilipoanza katika jimbo la Rakhine. Waislamu wanakabiliwa wanagamizi ya umati katika hujuma zinazofanywa na wanajeshi na mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada nchini Myanmar.