Unyanyasaji dhidi ya Waislamu waongezeka mno nchini Uingereza
Gazeti moja la nchini Uingereza limeripoti habari ya kuongezeka unyanyasaji na mashambulizi dhidi ya Waislamu nchini humo katika mwaka huu wa 2017.
Gazeti la Independent la nchini Uingereza limetoa ripoti maalumu na kuandika kuwa, mashambulizi na unyanyasaji wa Waislamu katika barabara na mitaa ya nchi hiyo imeongezeka kwa takriban asilimia 50 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita huku wanawake Waislamu wakiwa wahanga wakuu wa mashambulizi hayo yanayotokana na chuki dhidi ya Uislamu.

Gazeti hilo limeongeza kuwa, unyanyasaji huo umepelekea wanawake wengi Waislamu nchini Uingereza kubadilisha mavazi yao ya Kiislamu na badala ya kuvaa hijabu na vitambaa vya kusitiri nywele zao, sasa wameamua kutumia kofia.
Kundi moja linalofuatilia mashambulizi yanayotokana na chuki na husda nchini Uingereza limeripoti kuwa, zaidi ya thuluthi ya wahanga wa mashambulizi yanayotokana na chuki za kidini dhidi ya Uislamu katika mitaa ya Uingereza ni wanawake Waislamu hususan wale wanaovaa vazi la staha la Hijabu.
Wimbi la chuki na unyanyasaji dhidi ya Waislamu nchini Uingereza linazidi kuongezeka licha ya kwamba idadi ya Waislamu ni kubwa katika jamii ya nchi hiyo. Licha ya kuweko idadi hiyo kubwa ya Waislamu nchini Uingereza, lakini hadi leo hii wanaishi kwa wasiwasi kutokana na usalama mdogo.