Kuongezeka uhasama na chuki dhidi ya Waislamu barani Ulaya
Kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu na vitendo vya ukatili dhidi ya Waislamu katika nchi mbalimbali za Ulaya kumewatia wasiwasi viongozi wengi wa nchi za bara hilo juu ya matokeo ya mwenendo huo.
Farda Ataman, kamishna wa serikali ya shirikisho wa kupambana na ubaguzi wa rangi nchini Ujerumani, ametahadharisha kuhusu ubaguzi mkubwa wa rangi unaofanywa dhidi ya Waislamu na kusisitiza kuwa, uadui dhidi ya Waislamu umefikia kiwango cha kuwepo ulazima wa kuuchukulia hatua. Ataman ametoa wito pia wa kuwepo "mkakati mpana dhidi ya ubaguzi wa kidini". Afisa huyo wa serikali ya shirikisho ya Ujerumani amesema kuhusiana na suala hilo kwamba, mkakati wa kupambana na ubaguzi wa kidini inapasa ujumuishe kuzuia suala hilo na kuongeza uelewa, pamoja na kuongeza ulinzi wa kukabiliana na ubaguzi unaofanywa dhidi ya Waislamu.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti mpya uliofanywa na Shirika la Haki za Msingi la Ulaya (FRA) kuhusu ubaguzi dhidi ya Waislamu katika Umoja wa Ulaya, Waislamu nchini Ujerumani wamekumbwa na ubaguzi mkubwa zaidi wa rangi baada ya wenzao wa Austria.
Ujerumani ni miongoni mwa nchi za Ulaya ambazo zina idadi kubwa zaidi ya Waislamu, lakini licha ya kauli mbiu zote za nchi za Ulaya kuhusu kuwepo uhuru wa kuabudu na kutoa maoni, Waislamu wa nchi hiyo wanakabiliwa na mashinikizo, ubaguzi, maudhi na unyanyasaji mkubwa. Hali hiyo imeongezeka zaidi baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ya Oktoba 7, 2023 wakati Harakati ya Hamas iliposhambulia kusini mwa Israel.
Almaz Tefra, mtafiti wa masuala ya ubaguzi wa rangi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, amedokeza kuwa zaidi ya Waislamu milioni tano wanaishi nchini Ujerumani, lakini wanakabiliwa na upendeleo na ubaguzi wa rangi katika maisha yao ya kila siku. Tefra amesema, "kwa miaka kadhaa, Waislamu nchini Ujerumani wamekuwa wakikabiliwa na ubaguzi, chuki na wakati mwingine vitendo vya ukatili katika maisha yao ya kila siku."
Kwa mujibu wa takwimu za Polisi ya Makosa ya Jinai ya serikali ya Shirikisho ya Ujerumani, tangu ulipoanza mwaka huu hadi sasa, vimetokea vitendo zaidi ya 400 vya chuki dhidi ya waomba hifadhi na matukio zaidi ya 500 ya uhalifu dhidi ya waomba hifadhi na wahamiaji; ambayo mengi yao yalikuwa ya uchochezi uliofanywa na wafuasi wa mrengo wa kulia wenye misimamo mikali.
Kuhusiana na suala hili, kitambo si kirefu nyuma, mashirika ya kutetea haki za binadamu yalitahadharisha kuhusu kuongezeka maradufu uhalifu na matukio dhidi ya Waislamu na kueleza kwamba, upuuzaji wa viongozi wa Ujerumani juu suala hilo unatia wasiwasi. Shirika la CLAIM, linalojulikana kama taasisi rasmi ya nchini Ujerumani linalofuatilia uenezaji hofu juu ya Uislamu na chuki dhidi ya Waislamu, limeripoti ongezeko la asilimia 114 la uhalifu wa chuki dhidi ya Waislamu nchini humo.
Lakini si Ujerumani pekee, bali hata katika nchi nyingine za Ulaya, hali imekuwa ngumu zaidi kwa Waislamu. Sirpa Raoti, mkurugenzi wa Shirika la Haki za Msingi la Umoja wa Ulaya, anasema kuhusiana na hili: "Tunashuhudia ongezeko la kutisha la mwenendo wa ubaguzi wa rangi na upendeleo dhidi ya Waislamu barani Ulaya. Kwa hakika, nchi za Ulaya zimeifanya hali kuwa ngumu kwa maisha ya Waislamu. Kushika madaraka vyama vya mrengo wa kulia katika baadhi ya nchi za Ulaya zikiwemo Ujerumani na Austria ni moja ya sababu kuu za kushadidi ubaguzi na mashinikizo dhidi ya Waislamu".
Vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia barani Ulaya daima vimekuwa na misimamo dhidi ya Waislamu, na katika miaka ya hivi karibuni, vimekabiliana kivitendo na Waislamu katika nyanja mbalimbali za kisiasa na kijamii.
Kushambuliwa misikiti na vituo vya kidini vya Waislamu, kuwanyanyasa Waislamu wanaovaa mavazi ya Kiislamu, na kukosekana usawa katika upataji ajira na elimu ni mifano hai ya mashinikizo yanayowaandama Waislamu katika nchi za Ulaya. Hali hii imekuwa ikiongezeka, na kutokana na kuzidi kupata nguvu vyama vya mrengo wa kulia barani Ulaya, pamoja na kuendelea vita vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza hali hii imezidi kupamba moto.
Sirpa Raoti, Mkurugenzi wa Shirika la Haki za Msingi la Umoja wa Ulaya (EU) amesema: "Tunashuhudia ongezeko la kutisha la tabia ya ubaguzi wa rangi na upendeleo dhidi ya Waislamu barani Ulaya. Suala hili limepata nguvu zaidi kufuatia kuzuka mapigano Magharibi mwa Asia na kushadidishwa na kauli zisizo za kiutu na za chuki dhidi ya Uislamu za baadhi ya watu kote barani Ulaya".
Licha ya indhari zote hizi, inavyoonekana, ubaguzi wa rangi na hata ukatili dhidi ya Waislamu utaendelea barani Ulaya hadi pale viongozi wa nchi za bara hilo watakapochukua hatua madhubuti na za kivitendo za kuzuia siasa za kueneza chuki dhidi ya Waislamu barani humo.