Umoja wa Mataifa: Mwanamke mmoja huuliwa kila baada ya dakika 10
-
UN: Mwanamke mmoja anauawa kila baada ya dakika kumi
Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa jana Jumatatu ilisema kwamba karibu wanawake 50,000 waliuawa na jamaa zao mwaka wa 2024, kwa kiwango cha mwanamke mmoja kila baada ya dakika 10, na kuelezea masikitiko yake kwamba hakuna maendeleo yoyote yaliyopatikana katika kupambana na mauaji ya wanawake.
Mwaka jana, wanawake na wasichana 83,000 waliuawa kwa makusudi duniani kote, kwa mujibu na ripoti iliyotolewa na Ofisi ya Wanawake ya Umoja wa Mataifa na vilevile Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake.
Ripoti hiyo imeeleza kwamba 60% kati yao, yaani wanawake na wasichana 50,000, au wastani wa mauaji 137 kwa siku, waliuawa "na wapenzi wao au wanafamilia."
Kwa upande mwingine, ni 11% tu ya mauaji yaliyofanywa na wenzi wa karibu au wanafamilia dhidi ya wanaume.
Ripoti hiyo inasema, ingawa idadi hii ni ndogo kidogo kuliko takwimu iliyorekodiwa mwaka 2023, lakini haionyeshi kupungua idadi ya uhalifu uliofanywa dhidi ya wanawake, kwa sababu kwa kiasi kikubwa, inatokana na tofauti katika upatikanaji wa data kutoka nchi moja hadi nyingine.

Uhalifu huu wa mauaji ya wanawake na wasichana umerekodiwa katika mabara yote, lakini Afrika imeshuhudia tena idadi kubwa zaidi ya mauaji hayo mwaka jana, ikiwa na takriban visa 22,000.
Sarah Hendricks, mkurugenzi wa sera katika UN Women, amesema kwamba mauaji ya wanawake hayatokei peke yake, lakini mara nyingi huwa "sehemu ya mzunguko unaoendelea wa ukatili, kuanzia kwenye mienendo ya kudhibiti, vitisho na unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na kupitia mtandaoni."
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu, John Brandolino, amesema kwamba ripoti hiyo inakumbusha udharura wa kuboreshwa mikakati ya kuzuia na kuchukuliwa hatua dhidi ya jinai za mauaji ya wanawake.
Ameongeza kuwa: "Nyumba inasalia kuwa mahali hatari, na wakati mwingine eneo la mauaji, kwa wanawake na wasichana wengi kote duniani."