Kwa nini mataifa ya Ulaya yanaunga mkono chuki dhidi Uislamu?
(last modified Wed, 05 Feb 2025 02:39:49 GMT )
Feb 05, 2025 02:39 UTC
  • Kwa nini mataifa ya Ulaya yanaunga mkono chuki dhidi Uislamu?

Ikiwa ni katika muendelezo wa siasa za chuki dhidi ya Uislamu mwanasiasa mwenye uraia pacha wa Sweden na Denmark na mwenye chuki dhidi ya Uislamu, Rasmus Paludan kwa mara nyingine tena ameivunjia heshima Qur'ani Tukufu kwa kuchoma moto nakala ya kitabu hicho kitakatifu cha Waislamu katika mji mkuu wa Denmark, Copenhagen.

Paludan, mwenye umri wa miaka 43, mwasisi na kiongozi wa chama kinachopinga uhamiaji cha Stram Kurs, kwa mara nyingine tena ameughadhabisha umma wa Kiislamu kwa kufanya kitendo hicho cha kufuru nje ya ubalozi wa Uturuki nchini Denmark.

Video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii inamuonyesha Paludan akiivunjia heshima Qur'ani Tukufu, kitendo kinachokera sana Waislamu duniani kote. Uafriti huu mpya umefanyika katika hali ambayo, Mahakama ya Denmark mnamo Agosti mwaka 2023 iliamua kupiga marufuku vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu kufuatia taathira mbaya za hatua hizo.

Hatua ya mwanasiasa huyo mwenye misimamo ya kufurutu ada ya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu nchini Denmark inajiri siku chache baada ya mkimbizi wa Iraq, Salwan Momika aliyekuwa na tabia kama hiyo, kuangamizwa kwa kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake katika mji wa Sodertalje, Sweden mnamo Januari 30.

Sera ya chuki dhidi ya Uislamu imeshika kasi katika miaka ya hivi karibuni katika nchi za Ulaya na hata baadhi ya nchi hizo zimeunga mkono sera hii kwa kuchukua hatua na kupitisha sheria katika uwanja huo. Kupiga marufuku uvaaji wa hijabu katika nchi za Ufaransa, Ujerumani na Austria, kuwanyanyasa wanawake wanaovaa hijabu ya Kiislamu nchini Ufaransa na baadhi ya nchi nyingine za Ulaya, kueneza chuki dhidi ya Waislamu na kuwaita magaidi, pamoja na kutoa idhini ya kuichoma moto Qur'ani Tukufu katika nchi kama vile Uswidi, ni mambo ambayo kivitendo yameandaa uwanja wa Waislamu kutokuwa na amani na utulivu.

Salwan Momika aliyekuwa na tabia ya kuvunjia heshima Qur'ani aliuawa kwa kupigwa riisasi hivi kkaribuni

 

Nchi za Magharibi zimepitisha sera hizo huku zikikabiliwa na changamoto kubwa katika nyanja za kimaadili, kidini na kijamii katika miaka ya hivi karibuni, changamoto ambazo zimepelekea vyama vya mrengo wa kulia kurejea madarakani katika nchi nyingi za bara Ulaya.

Kwa hakika kuimarika kwa vyama hivyo barani Ulaya katika muktadha wa kushindwa kisiasa na kiuchumi kwa vyama tawala na hali mbaya ya kijamii na kiuchumi ya nchi hizo kumesababisha nguvu za mrengo wa kulia kuongezeka katika medani za kisiasa na kijamii ambapo utendaji kama vile kukabiliana na wahamiaji na chuki dhidi ya Uislamu ni miongoni mwa hatua ambazo zinachukuliwa na vyama hivyo.

Vyama vya mrengo wa kulia vya Ulaya vinachukulia uwepo wa Waislamu katika jamii za Ulaya kuwa ndio sababu ya pengo la utambulisho wa umoja na vinaamini kwamba, mafundisho ya Waislamu hayaendani na mawazo ya jamii ya Ulaya na kwa hivyo vikwazo vinapaswa kuongezwa dhidi yao.

Kwa upande mwingine, kuongezeka kwa idadi ya Waislamu katika nchi mbalimbali za Ulaya kumepelekea kuongezeka kupendwa Uislamu katika jamii hizo, ambapo vyama vya mrengo wa kulia haviko tayari kuvumilia hilo.

Katika miaka ya hivi karibuni, vyama hivyo vimejaribu kufikia malengo yao katika uwanja wa chuki dhidi ya Uislamu kwa kushinikiza vyombo vya utendaji na sheria vya nchi mbalimbali za Ulaya kupitisha sheria dhidi ya wahamiaji, kuandaa ghasia na mivutano dhidi ya Waislamu pamoja na kutayarisha marufuku za wazi na za siri kwa minajili ya kufikia malengo yao. Kuunga mkono uchomaji wa Quran pia kunathminiwa katika fremu hii.

Vitendo hivi vinafanyika katika hali ambayo, nchi za Ulaya zimekuwa zikidai kutetea uhuru wa kujieleza, uhuru wa mtu binafsi na haki za binadamu. Hata hivyo, katika matukio haya ya kuchomwa moto Qur'ani na mengine yaliyo dhidi ya Uislamu na Waislamu nchi hizo zimekuwa na msimamo wa kinafiki na kindumakuwili na hushikimana na misingi hiyo pale tu kunapokuweko maslahi yao na ya washirika wao.

Kuhusiana na suala hilo, Farhan Haq, msemaji wa Umoja wa Mataifa amesisitiza umuhimu wa kuhifadhiwa uhuru wa kusema kuwa ni haki ya msingi ya binadamu na kutangaza kwamba: Kuvunjiwa heshima vitabu vitakatifu na maeneo ya ibada pamoja na alama za kidini ni jambo lisilokubalika na linaweza kuchochea ghasia na vurugu.

Ukweli wa mambo ni kuwa, hivi sasa kukaririwa kitendo cha kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu kunaonyesha kwamba, nchi za Magharibi zikiwa na utendaji wa kindumakuwili zimetosheka tu na kutoa kauli mbiu nzuri kuhusu kushikamana na haki za binadamu. Mataifa hayo sio tu kwamba hayashughulishwi kabisa na suala kuvunjiwa heshima Waislamu bali hayana itikadi kabisa na suala hilo. Kimsingi ni kuwa, madola ya Magharibi yamekuwa yakifuatilia utekelezaji wa sera za chuki dhidi ya Uislamu katika mbinu na kalibu mbalimbali.