Nov 10, 2017 04:55 UTC
  • Al Abadi: Karbala inawahusu wanadamu wote

Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi amesema kuwa mapenzi ya watu kwa Karbala na Imam Hussein ni kielelezo kwamba tukio lililojiri katika eneo hilo linawahusu wanadamu wote na si makhsusi kwa dini au madhuhebu moja.

Haider al-Abadi ambaye alikuwa akizungumza kwa mnasaba wa shughuli ya Arubaini ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as), amesema kuwa, mawimbi ya watu walioelekea Karbala na mapenzi yao ya aina yake kwa Imam Hussein (as) ni ushahidi kwamba yaliyomsibu mtukufu huyo yanawahusu wanadamu wote na si wafuasi wa dini wala madhehebu fulani.

Haider al-Abadi

Waziri Mkuu wa Iraq ameongeza kuwa, harakati ya mapambano ya Imam Hussein ilikuwa mapinduzi ya kuwaondoa wanadamu katika minyororo na utumwa na kwamba ni wajibu wa Waislamu wote kuiga nyayo na mwenendo wa mtukufu huyo.

Jana tarehe 20 Safar mamilioni ya watu walishiriki katika maombolezo ya Arubaini ya mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 20 wameshiriki katika shughuli hiyo. 

Karbala, Iraq

Majlisi na shughuli ya siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume na masahaba zake watiifu ambao walijisabilia roho zao wakipambana na mtawala dhalimu Yazid bin Muawiya kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika ardhi ya Karbala nchini Iraq.

Tags