China: Myanmar na Bangladesh zishirikiane kutatua matatizo ya Waislamu wa Rohingya
Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi amezitaka serikali za Myanmar na Bangladesh kutatua matatizo ya Waislamu wa Rohingya, badala ya kusubiri utatuzi wa jamii ya kimataifa katika uwanja huo.
Kwa mujibu wa Wang Yi, nchi hizo zinatakiwa kufanya mazungumzo ya pande mbili kuhusiana na mgogoro unaowakabili Waislamu hao. Waziri wa Mambo ya Nje wa China ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Bangladesh, Abul Hassan Mahmood Ali mjini Dhaka, mji mkuu wa nchi hiyo.
Amesema kuwa, hatua za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inapasa zisaidie kuleta ushirikiano wa pande mbili hizo, ili ziweze kufanikisha kutatuliwa matatizo ya jamii hiyo ya Rohingya kwa njia za amani. Waziri wa Mambo ya Nje wa China amefanya safari ya siku mbili nchini Bangladesh kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa Asia na Ulaya unaofanyika nchini humo. Zaidi ya Waislamu laki nane wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar wamekimbilia Bangladesh kutokana na vitendo vya ukandamizaji vya jeshi la serikali kwa kushirikiana na Mabudha magaidi wa nchi hiyo. Akielezea suala hilo, Wang Yi amesema kuwa, suala hilo tata lazima lipatiwe ufumbuzi wa haraka.
Katika mazungumzo hayo na waandishi wa habari Abul Hassan Mahmood Ali, Waziri wa Mambo ya Nje wa Bangladesh amesema kuwa, nchi yake haiwezi kustahmili kubeba mzigo wa wakimbizi hao peke yake na kwamba Dhaka inafanya juhudi za kutatuliwa suala hilo kwa ushirikiano wa pande mbili na katika ngazi ya kimataifa. Ukandamizaji unaoenda sambamba na jinai za kutisha za mauaji ya kizazi dhidi ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar, ulianza tangu tarehe 25 Agosti mwaka huu, na kupelekea zaidi ya watu elfu sita kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa.