Sanders: Matamshi ya Trump kuhusu Waislamu yanakera
Mgombea tiketi ya chama cha Democratic kwa ajili ya kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais nchini Marekani, Bernie Sanders amekosoa vikali matamshi yanayotolewa na mgombea mwenzake wa chama cha Republican, Donald Trump dhidi ya Waislamu akisema mashambulizi dhidi ya Waislamu wote duniani kwa kutumia kisingizio cha matukio kama yale ya hivi majuzi mjini Brussels yanakasirisha na yanapingana na katiba ya Marekani.
Bernie Sanders amesema Donald Trump anayemiliki vilabu vya kamari na bilionea anayezusha mjadala mkubwa, anafanya mchezo wa kuigiza wa televisheni na kwamba anatumia matukio ya Brussels kama kisingizio cha kuchochea chuki dhidi ya Waislamu. Sanders amesisitiza kuwa, matamshi na mwenendo huo unaeneza hofu na woga katika jamii ya Marekani.
Mgombea huyo wa tiketi ya chama cha Domocratic kwa ajili ya uchaguzi wa rais wa Marekani amesema kuwa, kundi la kigaidi la Daesh ni genge ovu lililofanya uhalifu na jinai dhidi ya binadamu huko Ufaransa, Marekani na Ubelgiji lakini mapambano dhidi ya kundi hilo hayapasi kukiuka katiba ya Marekani.
Bernie Sanders amesema haipasi kuwapa watu kama Trump fusra ya kutumia matukio kama ya Ubelgiji kwa ajili ya kutumia vibaya matukio ya kusikitisha kama yale ya Brussels kuhujumu Waislamu wote duniani.