Sadiq Khan ataka kufutwa safari ya Trump nchini Uingereza
Meya wa mji wa London ameomba kufutwa ziara rasmi ya Rais Donald Trump wa Marekani nchini Uingereza.
Sadiq Khan ametoa taarifa kali leo akikosoa hatua ya Donald Trump ya kuzisamba upya video zinazochafua jina la Uislamu na kusisitiza kwamba video hizo zinapaswa kufuta.
Meya wa mji wa London ametaka kufutwa safari rasmi ya Rais huyo wa Marekani nchini Uingereza. Taarifa ya Meya wa London imeongeza kuwa Trump alitumia ukurasa wa twitter ili kulipa nguvu kundi moja lenye misimamo mikali ambalo msingi wake mkuu wa kuendelea kuwepo ni kueneza chuki katika jamii.
Awali Sadiq Khan alikuwa amemuomba Waziri Mkuu wa Uingereza, Bi Theresa May afute pendekezo lake la kumwalika rasmi Trump nchini humo.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza pia imetoa taarifa ikikosoa hatua hiyo ya Trump ya kuonyesha video hizo dhidi ya dini ya Uislamu.
Wakati huo huo Jeremy Corbyn kiongozi wa chama cha Labour nchini Uingereza ameitaja hatua hiyo ya Rais wa Marekani kuwa ni hatari na inayotishia jamii na kuitaka serikali ya London kulaani kitendo hicho.
Hatua ya Rais wa Marekani ya kuzisambaza kupitia ukurasa wake wa twitter video hizo tatu inayochochea chuki na kuchafua jina la Uislamu imezusha hasira kubwa za walimwengu katika maeneo mbalimbali duniani.
Awali video hizo tatu dhidi ya Uislamu na Waislamu zilirushwa mitandaoni na chama kidogo cha kibaguzi cha mrengo wa kulia nchini Uingereza, "Britain First".