Wabangali waandamana kulaani njama za kufuta Uislamu kuwa dini rasmi
Maelfu ya wananchi wa Bangladesh wamefanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo kukosoa kile walichokitaja kuwa njama za baadhi ya watu wanaojiita 'mashuhuri' nchini humo kutaka Uislamu usitambuliwe kuwa dini rasmi ya nchi hiyo.
Habari zinasema kuwa, wananchi zaidi ya elfu 3 waliandamana jana nje ya Msikiti wa Jamia wa jijini Dhaka baada ya Swala ya Ijumaa, kulaani azma wanayosema kuwa inakiuka sheria na katiba ya nchi ya kuitaka Mahakama Kuu nchini humo itangaze kuwa Uislamu sio dini rasmi ya nchi hiyo.
Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa, pendekezo hilo liliwasilishwa mahakamani na kundi la wananchi wanaojiita mashahuri nchini humo.
Azma hiyo ya kutaka kuifuta dini tukufu ya Kiislamu kuwa dini rasmi ya nchi hiyo inafanyika katika hali ambayo, zaidi ya asilimia 90 ya wananchi milioni 160 wa Bangaldesh ni Waislamu.
Licha ya kiongozi wa zamani wa kijeshi nchini humo H.M Ershad kutangaza Uislamu kuwa dini rasmi nchini Bangaldesh mwaka 1988, lakini Waziri Mkuu wa sasa Sheikh Hasina alitumia usekulari kama nguzo ya katiba ya nchi hiyo mwaka 2011.
Hata hivyo Uislamu ulibakia kuwa dini rasmi ya taifa.