Shaka na wasiwasi kuhusu uzima na utimamu wa akili wa Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i38665-shaka_na_wasiwasi_kuhusu_uzima_na_utimamu_wa_akili_wa_trump
Gumzo na mijadala kuhusu uzima wa akili wa Rais wa Marekani sasa imegeuka kuwa maudhui muhimu inayozungumziwa ndani na nje ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 08, 2018 04:23 UTC

Gumzo na mijadala kuhusu uzima wa akili wa Rais wa Marekani sasa imegeuka kuwa maudhui muhimu inayozungumziwa ndani na nje ya nchi hiyo.

Siku moja baada ya kuchapishwa kitabu kilichozusha rabsha na taharuki kiitwacho "Moto na Ghadhabu: Ndani ya Ikulu ya Trump" kwa kimombo "Fire and Fury: Inside the Trump White House", ambacho mwandishi wake Michael Wolff amesema Trump ni mtu mwenye tabia za kitoto, rais huyo wa Marekani amejitokeza na kudai kwamba yeye ni mtu mwenye kipawa cha juu kabisa. Kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, Donald Trump ameandika: "Mimi nimepiga hatua kutoka kuwa mfanyabiashara aliyefanikiwa mno na kuwa mwendeshaji maarufu wa vipindi vya televisheni na kufikia kuwa rais wa Marekani; tena basi ni kwa kushiriki uchaguzi kwa mara ya kwanza. Mimi nadhani kuwa hodari tu hakutoshi ili kuwa hivi, mimi ni mtu mtu kwenye kipawa cha juu kabisa, tena chenye uthabiti mkubwa".

Tabia za ajabuajabu na za kitoto za Trump

Wakati unakaribia kuwadia mwaka mmoja wa urais wa Donald Trump, mijadala imepamba moto kati ya wanasiasa, waandishi wa habari na wenye vipawa ndani ya jamii ya Marekani kuhusu kiwango cha uzima na utimamu wa akili wa rais wa nchi hiyo. Wakosoaji wa Trump kuanzia kundi kubwa la wanasiasa wa chama wa Democrat hadi vyombo vya habari wanaitakidi kuwa rais huyo wa Marekani hayuko sawa na thabiti kinafsi na kiakili na hana sifa za kuwa rais na Amiri Jeshi wa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo. Katika maelezo yaliyomo kwenye kitabu chake kilichomchukulia muda wa miezi kadhaa ya kuingia na kutoka Ikulu ya White House na kufanya mahojiano na washauri wa Trump, Michael Wolff ameandika: "watu wote ambao wamefanya kazi na Trump kwenye Ikulu ya White House wanakubaliana kwa pamoja juu ya suala moja, nalo ni kwamba rais ana tabia kama za mtoto mdogo".

Michael Wolff

Kwa mtazamo wa wakosoaji, hata jibu na radiamali aliyoonyesha Trump kuhusiana na shaka anayotiliwa juu ya uzima na utimamu wake wa akili inaonyesha kuwa ana tabia za kitoto, kutokana na maelezo yake ya kujitangaza kuwa yeye ni mtu mwenye kipawa cha juu kabisa. Baadhi ya wakosoaji wengine wakiwemo wataalamu wa Saikolojia nchini Marekani wanaitakidi kuwa Trump anakaribia kupata ugonjwa wa kurukwa na akili na anasumbuliwa na hali mbaya mno ya ghururi na kujiona.

John Garamendi, mbunge wa chama cha Republican katika Kongresi ya Marekani anasema, yeye na wabunge wengine wengi wa chama hicho wanakabiliwa na shaka kubwa kuhusu uwezo wa Donald Trump wa kushikilia wadhifa wa urais wa nchi hiyo.

Harakati zisizo za kawaida za Trump; kulia ni Rais Xi Jinping wa China akimshangaa

Alaa kulli haal, kutokana na kuibuka masuala kama hayo, hivi sasa duru za kisiasa na za vyombo vya habari zinazungumzia hoja ya kutumiwa kifungu cha nyongeza cha 25 cha katiba ya Marekani kinachohusu kuondolewa rais madarakani. Kwa mujibu wa kifungu hicho ikiwa Baraza la Mawaziri likiongozwa na Makamu wa Rais litapiga kura kuthibitisha kuwa rais hana uwezo kimwili au kiakili wa kuendesha masuala ya nchi, utaratibu uliowekwa utatumika ili kumwondoa madarakani. Bila shaka hadi sasa kifungu hicho cha katiba ya Marekani hakijawahi kutekelezwa kuhusiana na rais yeyote wa nchi hiyo, lakini uwezekano wa kutumika kifungu hicho cha nyongeza cha 25 cha katiba ili kumuuzulu Trump umezidi kupata nguvu kutokana na mijadala iliyopamba moto kuhusiana na mwenendo na tabia za ajabuajabu alizoonyesha kiongozi huyo katika miezi ya hivi karibuni.../