Joto lilivunja rekodi duniani mwaka 2017, wasiwasi kuhusu mustakabali
Mwaka uliopita wa 2017 umetajwa kuwa mwaka uliovunja rekodi ya joto kali zaidi katika historia ya sayari ya dunia pasina kuwepo tukio la El Niño huku kukiwa na wasi wasi kuwa hali itazidi kuwa mbaya katika miaka ijayo.
Wataalamu wanasema mabadiliko ya tabia nchi yanayochangiwa na ongezeko la uchafuzi wa hewa kutokana na shughuli za wanadamu ndio sababu ya ongezeko la joto duniani. Miaka ya 2015, 2016 na 2017 imethibitishwa kuwa miaka mitatu iliyovunja rekodi ya kuwa na joto la kupindukia katika historia.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya hali ya joto duniani iliyotolewa na Shirika la Utabiri wa Hali ya hewa Duniani WMO ambalo limesema mwaka 2016 bado unashikilia rekodi ya juu ya joto duniani wakati wa kipindi cha El Niño ambayo inaweza kupandisha kiwango cha joto cha mwaka kimataifa.
Tathimini ya kina ya WMO katika vituo vitano vya kimataifa vya ukusanyaji data, imeonyesha kwamba kiwango cha joto duniani mwaka 2017 ni wastani wa nyuzi joto 1.1 kikiwa ni juu ya ilivyokuwa kabla ya maendeleo ya viwanda.
Katibu mkuu wa WMO Petteri Taalas amesisitiza kwamba mwenendo wa muda mrefu wa ongezeko la joto ni jambo linalotia wasiwasi kuhusu mustakhbali wa dunia. Wataalamu wanasema kuna haja ya kuchukuliwa hatua za kuzuia uchafuzi wa mazingira ili kuzuia ongezeko la joto duniani. Hii ni katika hali ambayo Rais Donald Trump wa Marekani ameonidoa nchi yake katika mkataba wa kimataifa wa kuzuia uchafuzi wa hewa katika hali ambayo Marekani ni kati ya nchi zinazoongoza katika uchafuzi wa mazingira na hivyo kusababisha mabadiliko ya tabinchi na ongezeko la joto duniani kutokana na viwanda vyake.
Uchafuzi huo wa mazingira mbali na kupelekea ongezeko la joto duniani pia ni chanzo cha majanga makubwa kama vimbunga, mafuriko, mawimbi na ukame.