Sep 12, 2024 07:26 UTC
  • Mdahalo wa kwanza wa uchaguzi wa rais wa Marekani kati ya Harris na Trump

Mgombea wa chama cha Demokrat Kamala Harris na mgombea wa chama cha Republican Donald Trump katika uchaguzi wa urais wa Marekani wa Novemba 5, 2024, walishiriki katika mdahalo wao wa kwanza siku ya Jumanne usiku, Septemba 10.

Wagombea hao wawili waliibua masuala mbalimbali ya ndani na nje ya nchi katika mdahalo huo wa dakika 90 wa televisheni ulioandaliwa na Shirika la Utangazaji la NBC katika Kituo cha Kitaifa cha Katiba huko Philadelphia, Pennsylvania.

Kwa mujibu wa utafiti wa shirika la utangazaji la CNN, asilimia 63 ya watazamaji wa mdahalo wa kwanza kati ya wagombea wawili wa uchaguzi wa rais wa Marekani walisema kuwa Kamala Harris alifanya vizuri zaidi kuliko Donald Trump. Kulingana na utafiti huu, ni asilimia  37 tu  ya watazamaji wa mdahalo huu walioamini kuwa Trump alimshinda Harris.

Kabla ya utafiti huu, asilimia 50 ya wapiga kura wa Marekani waliamini kwamba Harris angeshinda mdahalo na wengine asilimia 50 walisema kuwa Trump angefanya vizuri katika mdahalo huo. Nukta muhimu hapa ni kwamba kulingana na uzoefu wa awali wa ushawishi wa mdahalo miongoni mwa wapiga kura,  kwa kawaida mgombea ambaye huongoza katika midahalo ana nafasi nzuri ya kushinda uchaguzi wa urais.

Katika mdahalo huo wa kwanza kati ya Harris na Trump, kila mmoja alifanya juhudi kubwa kuuharibu kisiasa upande wa pili. Harris alijaribu kuonyesha kuwa iwapo Trump atachaguliwa, huo utakuwa mwendelezo wa utawala wake wa awali, na Trump akajaribu kuonyesha utawala wa Harris utakuwa mwendelezo wa utawala wa Biden. Pamoja na hayo, kwa mtazamo wa wapiga kura wa Marekani, tawala zote mbili za Trump na Biden zimefeli.

Biden (kushoto) na Trump

Wakati wa mdahalo huo, Harris, ambaye aliwahi kuwa mwanasheria mkuu wa California, alitaka kumuonyesha mpinzani wake kama tishio kwa demokrasia na mafanikio ya Marekani huko nyuma, na kwa upande mwingine, Trump akiwa kama bilionea katika mfumo wa kibepari wa Marekani alimtuhumu Harris kuwa ni mkomunisti.

Inaonekana kwamba sisitizo la wagombea hao wawili wa uchaguzi wa rais wa Marekani kuhusu masuala ya kiuchumi ni kutokana na unyeti wa suala hili kwa raia wa Marekani, ambao hali yao ya kiuchumi na kimaisha inazidi kuwa mbaya.

Katika uga wa sera za kigeni, maudhui kuhusu utawala wa Israel, vita vya Gaza, operesheni ya  Kimbunga cha Al-Aqsa mnamo Oktoba 7, 2023, Iran na vita vya Ukraine yalikuwa maswali ya mdahalo wa kwanza kati ya Harris na Trump.

Harris alisema Marekani itaendelea kuunga mkono kile alichosema ni haki ya Israel ya kujilinda, lakini  akaongeza kuwa vita lazima viishe mara moja. Kwa upande mwingine, Trump kimsingi alitilia shaka kauli za Harris na kusisitiza kuwa: "Harris anaichukia Israel na iwapo atachaguliwa, Israel itatoweka ndani ya miaka miwili. Aidha alidai kwamba kama angekuwa rais, vita vya Gaza havingetokea kwa njia yoyote ile. Pia amedai kuwa kama angekuwa rais, vita vya Ukraine havingetokea kwa sababu Marekani haikuwa na tatizo na Rais Putin wa Russia. Trump aidha alikariri madai yake dhidi ya Iran huku akikosoa  sera za utawala wa Biden kuhusu Iran.

Kwa ujumla, kama ilivyotarajiwa, inaonekana kwamba mdahalo wa kwanza kati ya  Harris na  Trump umemalizika kwa ushindi wa Harris.

Mdahalo wa kwanza wa uchaguzi wa Rais wa Marekani mwaka huu ulifanyika  kati ya Donald Trump na Joe Biden ambaye awali alikuwa mgombea wa Chama cha Demokrat. Mdahalo huo ulimalizika kwa ushindi wa Trump kutokana na udhaifu  wa kiakili na kisaikolojia wa Biden jambo ambalo lilipelekea chama cha Demokrat kumshinikiza Biden ajiondoe na kumuachia Harris agombee urais.  Katika mdahalo wa Jumanne Harris aliweza kuonyesha utendaji bora na kuwasilisha misimamo yenye mantiki zaidi kinyume na alivyokuwa Biden.

Kabla ya mdahalo wa juzi, Trump alianzisha vita vya kisaikolojia dhidi ya Harris na kudai kwamba alikuwa na uwezo dunia wa kiakili. Lakini kwa ujumla Harris alionekana kuwa na uwezo mkubwa zaidi ya Trump. Pamoja na hayo Harris bado hajapata umaarufu wa kutosha wa kumhakikishia ushindi katika uchaguzi wa Novemba 5.

Tags