Nusu ya Wamarekani wanaamini Trump hana akili timamu
Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni yanaonyesha kwamba, nusu ya raia wa Marekani wanaamini kwamba, Rais Donald Trump wa nchi hiyo hana mlingano wa akili.
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na gazeti la Washington Post na televisheni ya ABC ya nchi hiyo, unaonyesha kwamba asilimia 50 ya raia wa Marekani wanaamini kuwa, rais huyo hana mlingano sawa wa akili, huku asilimia 58 wakiwa pia hawaridhii namna anavyoongoza nchi. Kadhalika uchunguzi huo unaonyesha kwamba asilimia 60 ya Wamarekani wanapinga kikamilifu mpango wa Trump wa kujengwa ukuta wa mpakani kati ya Marekani na Mexico.
Matokeo hayo yamezidi kubainisha kwamba, asilimia 73 ya raia wa nchi hiyo kinyume na madai ya Trump kwamba ni mwerevu sana, hawaoni ukweli wa jambo hilo. Uchunguzi huo ulifanywa kuanzia tarehe 15 hadi 18 ya mwezi huu na kuwashirikisha watu 10,000 nchini humo. Hivi karibuni na ikiwa ni mwaka mmoja umepita tangu aingie ikulu ya White House, kumeenea habari mbalimbali juu ya tabia na maneno yasiyo ya busara ya Rais Donald Trump, kiasi cha kuwafanya wataalamu wa saikolojia kuamini kuwa rais huyo hana akili timamu. Kadhalika watalaamu hao wametangaza kutokuwa na imani na uongozi wa mtawala huyo wa Marekani.