IAEA na EU zatetea tena makubaliano ya nyuklia ya JCPOA
Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na Umoja wa Ulaya (EU) zimetetea tena makubaliano ya nyuklia ya JCPOA baina ya Iran na nchi za kundi la 5+1.
Msimamo huo umebainishwa katika kikao cha sita cha kila mwaka kilichofanyika jana Alkhamisi mjini Vienna kati ya maafisa wa ngazi za juu wa pande hizo mbili.
Taarifa iliyotolewa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki imesema kuwa, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini ataendelea kuwasiliana na wakala huo kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa makubaliano hayo ya nyuklia ya kimataifa.
Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na Umoja wa Ulaya zimekuwa zikitangaza uungaji mkono wao kwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Hadi sasa wakala huo umetoa ripoti 9 ukithibitisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeheshimu na kutekeleza makubaliano hayo.
Makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambayo yalitiwa saini baina ya Iran na nchi sita wanachama wa kundi la 5+1 yaani Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, China, Russia na Marekani yalianza kutekelezwa Januari mwaka 2016 lakini serikali ya Washington ambayo pia iliyatia saini, imekuwa ikikiuka makubaliano hayo.
Kinyume na nchi nyingine wanachama wa kundi la 5+1, Rais Donald Trump wa Marekani anayataja makubaliano hayo ya kimataifa ambayo Marekani yenyewe iliyaidhinisha na kuyatia saini kuwa ni 'makubaliano mabaya zaidi' akitoa wito wa kuvunjiliwa mbali, suala ambalo linapingwa na nchi zote duniani.