FAO yatahadharisha kuhusu kuzidi ukosefu wa usalama wa chakula Yemen
(last modified Thu, 01 Mar 2018 07:30:28 GMT )
Mar 01, 2018 07:30 UTC
  • FAO yatahadharisha kuhusu kuzidi ukosefu wa usalama wa chakula Yemen

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetahadharisha kwamba, hali ya ukosefu wa usalama wa chakula inazidi kuwa mbaya huko nchini Yemen.

Taarifa ya FAO imeeleza kwamba, ukosefu wa usalama wa chakula nchini Yemen unazidi kuongezeka siku baada ya siku katika nchi hiyo na kwamba, hali hiyo ni mbaya ikilinganishwa na nchi nyingine ambazo zinakabiliwa na vita na machafuko. 

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa katika nchi 26 duniani imefahamika kwamba, mamilioni ya watu katika nchi za Yemen, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Somalia, Syria na Afghanistan wanakabiliwa na njaa na ukosefu wa usalama wa chakula.

Wakimbizi wa Somalia wakipatiwa chakula cha msaada

Inaelezwa kuwa, Wayemeni milioni 22 na laki mbili wanahitajia misaada ya chakula na kwamba milioni 8 na laki nne miongoni mwao wanakaribia kukumbwa na baa la njaa.

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, hivi karibuni José Graziano da Silva Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO alitangaza kwamba, vita, machafuko na ukame ni miongoni mwa sababu zilizochangia kuongezeka kwa idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa ulimwenguni.

Ripoti zinaonyesha kuwa, idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa ulimwenguni iliongezeka mwaka 2016 na kufikia milioni 815 ikilinganishwa na watu milioni 777 katika mwaka wa kabla yake.

Tags