Watu milioni 66 wanakabiliwa na uhaba wa chakula Pembe ya Afrika
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Jumuiya ya Kiserikali ya Maendeleo ya Afrika Mashariki IGAD zimesema katika ripoti yao mpya kwamba, watu milioni 66.7 katika eneo pana la Pembe ya Afrika hawana usalama wa chakula.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa, watu milioni 39.1 miongoni mwa watu milioni 66.7 wanaokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na katika viwango vya kutisha wanatoka katika nchi 6 kati ya 8 wanachama wa jumuiya ya IGAD.
FAO na IGAD zimesema nchi hizo sita wanachama wa IGAD ni Djibouti, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda. Aidha ripoti hiyo imesema nchi nyingine zinazosumbuliwa na ukosefu wa usalama wa chakula katika kanda hiyo ni Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ripoti hiyo ya pamoja ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Mashariki mwa Afrika na Pembe ya Afrika IGAD na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) imeongeza kuwa, mamilioni ya watoto katika eneo hilo la Pembe ya Afrika wanasumbuliwa na utapiamlo.

Hata hivyo ripoti hiyo inaashiria kupungua kwa idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba wa chakula Pembe ya Afrika kwa asilimia 11; yaani kutoka watu milioni 66.7 mwezi uliopita wa Juni ikilinganishwa na watu milioni 74.9 mwezi Mei mwaka huu.
Kwa mujibu wa FAO, takriban watu milioni 700, yaani asilimia 10 ya idadi ya watu duniani, wanalala njaa kila usiku. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linasema nchi 45 duniani, zikiwemo 33 za Afrika zinahitaji msaada wa dharura wa chakula kutoka nje.