Mar 08, 2018 01:41 UTC
  • UN: Tuna wasi wasi mauaji ya kimbari yamefanyika Myanmar

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza juu ya wasi wasi mkubwa alionao kwamba yumkini mauaji ya kimbari yamefanywa dhidi ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar tangu Agosti mwaka jana 2017.

Akihutubia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa hapo jana Jumatano, Zeid Ra’ad al-Hussein ameongeza kuwa, ripoti za kuharibiwa maeneo tofauti ya mkoa wa Rakhine hususan makazi ya Waislamu wa Rohingya, ni jaribio la makusudi la vyombo vya dola, la kutaka kuficha ukweli kuhusu jinai dhidi ya binadamu.

Amesema tangazo la hivi karibuni la serikali ya Myanmar kwamba itawapandisha kizimbani wanajeshi saba na askari polisi watatu kwa mauaji ya Warohingya kumi, halitoshi na kwamba hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa.

Nyumba za Warohingya zilizoteketezwa moto mkoani Rakhine

Hii ni katika hali ambayo, Jumanne iliyopita, Andrew Gilmour, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia masuala ya haki za binadamu alisema: "Matokeo ya safari yangu ya hivi karibuni ya siku nne katika kambi za wakimbizi wa Kirohingya nchini Bangladesh yanaonyesha kuwa, Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar wangali wanakabiliwa na mauaji yaliyoratibiwa kwa ajili ya kuitokomeza jamii hiyo kikamilifu."

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa, mbali na wengine zaidi ya laki saba kulazimishwa kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh, tangu Agosti 25 mwaka jana, lilipoanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo. 

Tags