Khoshroo: Iran inaunga mkono mapambano halali ya Wapalestina
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, Iran inaunga mkono mapambano halali ya wananchi wa Palestina yenye lengo la kuwa na mamlaka kamili na kuunda nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa Beitul-Muqaddas Mashariki.
Gholamali Khoshroo amesema hayo katika kikao cha mabalozi na wawakilishi wa kudumu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York na kulaani vikali jiani za hivi karibuni za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, tangu Machi 30 mwaka huu hadi sasa Wapalestin 111 wameuawa shahidi na wengine elfu kumi kujeruhiwa.
Gholamali Khoshroo ameashiria mauaji ya Wapalestina 60 katika siku ya kufunguliwa ubalozi wa Marekani mjini Quds iliyosadifiana na kumbukumbu ya mwaka wa 70 tangu kuasisiwa utawala vamizi wa Israel katika ardhi za Palestina na kusema kuwa, siku hiyo ilikuwa ni fedheha kubwa kwa Ulimwengu wa Kiislamu.
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kutumia suhula zote zilizonazo kwa ajili ya kuchukua hatua zinazofaa na za maana kuiunga mkono kadhia ya Palestina.