Pigo jingine dhidi ya Marekani katika Umoja wa Mataifa kuhusu Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i45856-pigo_jingine_dhidi_ya_marekani_katika_umoja_wa_mataifa_kuhusu_palestina
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, katika fremu ya kuunga mkono taifa madhulumu la Palestina, limepitisha kwa wingi wa kura azimio la kulaani vikali jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina na kwa utaratibu huo, Marekani, kwa mara nyingine tena, imepata pigo na kugonga mwamba katika jitihada zake za kulaani Harakati ya Mapambanao ya Kiislamu ya Palestina, Hamas.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jun 14, 2018 23:50 UTC
  • Pigo jingine dhidi ya Marekani katika Umoja wa Mataifa kuhusu Palestina

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, katika fremu ya kuunga mkono taifa madhulumu la Palestina, limepitisha kwa wingi wa kura azimio la kulaani vikali jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina na kwa utaratibu huo, Marekani, kwa mara nyingine tena, imepata pigo na kugonga mwamba katika jitihada zake za kulaani Harakati ya Mapambanao ya Kiislamu ya Palestina, Hamas.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika kikao cha dharura , Jumatano usiku liliitisha kikao cha kujadili hali ya mambo katika Ukanda wa Ghaza, ambapo lilipitisha kwa wingi wa kura rasimu ya azimio lililopendekezwa na Algeria na Uturuki kwa niaba ya nchi za Kiislamu kuhusu uungaji mkono wa kimataifa wa Palestina. Azimio hilo liliungwa mkono na nchi 120, likapingwa na nchi 120 huku nchi 45 zikijizuia kupiga kura.

Katika kikao hicho, Marekani ilishindwa kupata uungaji mkono kwa azimio lake dhidi ya Harakati ya Hamas. Katika azimio hilo Marekani ilikuwa imetaka harakati hiyo ya kupigania ukombozi wa Palestina ilaaniwe kwa kuvurumisha maroketi kutoka Ghaza kuelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel). Ni nchi 62 zilizounga mkono azimio hilo la Marekani huku nchi 48 zikilipinga na nchi 42 zikijizuia kupiga kura.

Nikki Haley, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amelalamikia vikali hatua ya kutopitishwa azimio hilo. Yaliyojiri katika kikao hicho cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni pigo jingine kubwa kwa sera za ubabe za Marekani katika uga wa kimataifa.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Marekani imepata pigo mara kadhaa kutoka jamii ya kimataifa ambayo inapinga sera zake za kuunga mkono utawala haramu wa Israel unaoendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina.  Matukio ya juzi katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yanaonyesha wazi kuwa, kinyume na madai ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu kile anachodai kuwa eti ni nguvu za nchi yake katika uga wa kimataifa, hivi sasa Washington inazidi kutengwa zaidi duniani. 

Trump amekuwa akichukua misimamo ya ubabe na ya upande mmoja katika sera za kimataifa katika kufikia malengo yake haramu kuhusu masuala mbali mbali ya kimataifa ikiwemo kadhia ya Palestina. Sera za Trump haziendi sambamba na ukweli wa mambo katika uga wa kimataifa na hakuna shaka zitapelekea kuongezeka kwa kasi kutengwa Marekani katika uga wa kimataifa. 

Kufuatia mashinikizo ya Wazayuni na utawala haramu wa Israel, Trump, aliutambua mji wa Quds (Jerusalem) kuwa eti ni mji mkuu wa utawala huo ghasibu na akahamishia ubalozi wa Marekani katika mji huo kutoka Tel Aviv, hatua ambayo imelaaniwa vikali kimataifa  na hata imepingwa na waitifaki wake wakuu barani Ulaya. Mbali na hayo, Marekani imeunga mkono wazi wazi jinai za utawala katili wa Israel ambao umewaua Wapalestina zaidi ya 125 kuanzia Machi 30 hadi sasa katika Ukanda wa Ghaza.

Jinai za kivita zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wasio na hatia

Wapalestina hao waliuawa wakati wakishiriki katika maandamano ya amani ya 'Haki ya Kurejea' katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na Israe. Hii ni katika hali ambayo mashirika ya kutetea haki za binadamu yamebaini wazi kuwa mauaji yaliyotekelezwa na Israel dhidi ya raia hao wa Palestina ni jinai za kivita.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch linasema: "Hatua za Israel katika kukabiliana na waandamanaji wa Ukanda wa Ghaza ni jinai ya kivita. Kutumia mabavu na silaha dhidi ya waandamanaji ambao si tishio kwa Waisraeli kumepelea kuuawa au kujeruhiwa idadi kubwa ya Wapalestina.

Mwanzoni mwa mwezi Juni pia,rasimu ya azimio la Marekani ambalo lilikuwa linalenga kuarifisha Hamas kama mhusika wa masaibu ya Ghaza pasina kutaja jinai za utwala haramu wa Israel katika eneo hilo, lilipingwa katika hatua isiyo na kifani ya wanachama wote wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Viongozi wa G7 katika kikao chao cha hivi karibuni Canada

Robert Malley, mwanachama wa zamani wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani anaamini kuwa siasa za upande mmoja za Rais Donald Trump wa Marekani zimepelekea nchi hiyo kutengwa katika ngazi za kimataifa. Msimamo wa hivi karibuni wa nchi wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umethibitisha wazi kuwa licha ya kukabiliwa na vitisho vya Marekani lakini haziko tayari kusalimu amri mbele ya siasa za mabavu na za ulazimishaji za nchi hiyo ya kibeberu wala kukubali matakwa yake yaliyo nje ya misingi ya sheria. Kwa kadiri kwamba nchi hiyo sasa imetengwa kwa namna ambayo ilikuwa haijawahi kushuhudiwa katika taasisi muhimu za kimataifa kama vile Baraza la Usalama, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kundi la nchi tajiri duniani G7 na nchi zinazoinukia kiuchumi za G20. Hii ni katika hali ambayo utawala haramu wa Israel pia umetengwa katika taasisi muhimu za kimataifa ukiwemo Umoja wa Matifa na kuhesabiwa kuwa utawala unaochukiwa zaidi katika taasisi hizo kutokana na jinai za kivita na kigaidi unazozitekeleza dhidi ya watu wasio na hatia wa Palestina.