Jul 06, 2018 13:33 UTC
  • Madaktari wathibitisha Waislamu Myanmar wametendewa jinai za kuogofya

Jumuiya ya Madaktari Watetezi wa Haki za Binadamu (PHR) imethibitisha ripoti za jinai za kuogofya wanazotendewa Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar.

Waislamu Warohingya walionusurikia maangamizi ya kimbari yanayoungwa mkono na serikali ya Myanmar na ambao wamepata hifadhi katika  kambi za wakimbizi katika nchi jirani ya Bangladesh wamewasimulia madaktari watetezi wa haki za binadamu masaibu waliokumbana nayo. Wakizungumza katika kambi ya wakimbizi ya Cox's Baza, Waislamu Warohingya wamesimulia nama walivyoteswa na kukandamizwa na jeshi huku nyumba zao zikiteketezwa na hivyo kuwalazimu kuondoka katika ardhi zao za jadi na kutafuta hifadhi nchini Bangladesh.

Madaktari Watetezi wa Haki za Binadamu wanasema wamewachunguza kitaalamu wakimbizi na kubainisha kuwa ni kweli wanavyosema kuwa wamekandamizwa na kuteswa na wanajeshi wa Myanmar. Utafiti wa madaktari hao uliwaangazia wakimbizi kutoka kijiji cha Chut Pyin katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar ambapo wakaazi Waislamu wa kijiji hicho walilazimika kukimbia baada ya wanajeshi kuwafyatulia risasi  raia, kuwabaka wanawake na kuteketeza moto nyumba zao.

PHR inasema kijiji cha Chut Pying ni mfano wa wazi wa kampeni ya mauaji nchini Myanmar ambayo inatekelezwa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Warohingya. Jumuiya hiyo imesema waliyotendewa Warohingya yanapaswa kuchunguzwa kama jinai dhidi ya binadamu.

Kijiji cha Waislamu kilichoteketezwa moto nchini Myanmar

Wimbi jipya la jinai dhidi ya Waislamu Rarohingya  lilishika kasi tangu tarehe 25 mwezi Agosti mwaka jana. Hadi sasa  jinai hizo zimepelekea kuuliwa Waislamu zaidi ya elfu sita na kujeruhiwa maelfu ya wengine huku wengine karibu laki nane wakilazimika kuwa wakimbizi katika nchi jirani ya Bangladesh.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein amesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya jeshi nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

Zeid Ra'ad Al Hussein anasisitiza kwamba, kuna udharura wa kufika katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na kufanya uchunguzi kuhusu ukatili unaofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu.

Tags