Kamal Kharrazi: Ulimwengu usimame na kukabiliana na ubeberu wa Marekani
Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Uhusiano wa Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa hili ni vya kidhulma na kuongeza kwamba, jamii ya kimataifa inapaswa kusimama kidete na kukabiliana na vikwazo hivyo.
Dakta Kamal Kharrazi amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari pambizoni mwa mkutano wa Baraza la Saba la Kimataifa la Amani mjini Beijing China na kueleza kuwa, Marekani si tu kwamba, inaikwamisha Iran tu, bali ulimwengu kwa ujumla ikiwemo China.
Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Uhusiano wa Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema bayana kwamba, hii leo ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na hatua za upande mmoja za Marekani ni jambo ambalo linahisika zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule.

Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Uhusiano wa Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, lengo la kila mazungumzo ni kutaka kuleta hali ya kuaminiana na kuongeza kuwa, kila mara Iran ilipoingia katika mazungumzo na Marekani kama kuhusiana na Afghanistan na makubaliano ya nyuklia haikupata isipokuwa natija ambayo ni kinyume na matarajio.
Dakta Kharrazi amesema kuwa, wananchi wa Iran wana hoja na matukio mengi ya kuwafanya wasiiamini Marekani.
Dakta Kharrazi amehoji kwa kusema, wakati serikali ya Marekani inapokiuka makubaliano ambayo imeyatia saini yenyewe, vipi watu wataiamini nchi kama hii?
Khrarazi ameitaja Iran pia kuwa nchi yenye amani na uthabiti zaidi miongoni mwa nchi za Mashariki ya Kati.