Jul 19, 2018 15:37 UTC
  • UN: Myanmar ingali inawatendea jinai Waislamu wa Rohingya

Wachunguzi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema Waislamu wa jamii ya Rohingya wangali wanafanyiwa jinai za kuogofya na wanajeshi wa Myanmar wakishirikiana na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada.

Maafisa hao wa Umoja wa Mataifa wametoa taarifa hiyo leo baada ya kumalizi ziara ya siku tano katika kambi ya Kutupalong wilayani Cox's Bazar nchini Bagladesh, na kufanya mahojiano na wakimbizi Waislamu wa Rohingya waliowasili katika kambi hiyo hivi karibuni.

Wanachama wa Jopo Huru la Kimataifa la Uchunguzi la UN wamesema wakimbizi hao wamewaeleza kuhusu namna walivyotendewa jinai na haki zao kukiukwa mkoani Rakhine, katika hali ambayo serikali ya Myanmar imekuwa ikidai kuwa mambo yametengamana na kuwataka wakimbizi hao kurejea nyumbani.

Wiki iliyopita, Tume ya Kiislamu ya Haki za Binadamu (IHRC) ilisema inataka wakuu wa kijeshi na kiserikali nchini Myanmar wafikishwe katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kujibu mashtaka ya kutenda jinai dhidi ya jamii ya Waislamu Warohingya.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein: Uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

Ilisema Jeshi la Myanmar na Mabudha wenye misimamo mikali wameachwa kuendelea na jinai zao ikiwa ni pamoja na kuua, kubaka wanawake na hata kuwateketeza moto watoto wadogo, jambo ambalo limepelekea Waislamu Warohingya kuondoka katika ardhi zao za jadi ili kuokoa maisha yao.

Wimbi jipya la jinai dhidi ya Waislamu wa Rarohingya lilishika kasi tangu tarehe 25 mwezi Agosti mwaka jana. Hadi sasa  jinai hizo zimepelekea kuuliwa Waislamu zaidi ya elfu sita na kujeruhiwa maelfu ya wengine huku wengine karibu laki nane wakilazimika kuwa wakimbizi katika nchi jirani ya Bangladesh.

Tags