Papa Francis: Jamii ya kimataifa izuie maafa ya binadamu Idlib
(last modified Mon, 03 Sep 2018 03:32:34 GMT )
Sep 03, 2018 03:32 UTC
  • Papa Francis: Jamii ya kimataifa izuie maafa ya binadamu Idlib

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis ameitaka jamii ya kimataifa itumie njia za kidiplomasia na mazungumzo kuzuia maafa ya binadamu katika mkoa wa Idlib nchini Syria.

Papa Francis amesema kuwa, kuna hatari ya kutokea maafa ya binadamu katika mkoa huo na kwamba, jamii ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua za kuzuia maafa hayo. 

Kiongozi wa Kanisa Katoliki alikuwa tayari ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za pamoja za kurejesha amani nchini Syria na maeneo mengine ya dunia yanayosumbuliwa na machafuko. 

Mkoa wa Idlib nchini Syria unadhibitiwa na magaidi wanaoungwa mkono na nchi za Magharibi.

Mkoa wa Idlib ndio wa mwisho nchini Syria ambao ungali unadhibitiwa na makundi ya kigaidi yanayosaidiwa na nchi za Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu kama Saudi Arabia. Jeshi la Syria na waitifaki wake wameanzisha operesheni kubwa ya kukomboa eneo hilo na kuwatimua kikamilifu magaidi hao.