Maafisa wa zamani wa serikali Marekani wamtaka Trump arejee kwenye JCPOA
Zaidi ya maafisa 50 wa zamani wa masuala ya usalama, siasa na jeshi wa Marekani wamesisitiza tena udharura wa nchi hiyo kurejea katika makubaliano ya nyuklia na Iran, kwa kifupi JCPOA.
Maafisa 53 wa zamani wa Marekani kutoka vyama vyote viwili vya Republican na Demokratic walitoa taarifa jana Jumapili wakitangaza kuwa: Siasa za Donald Trump kuhusu Iran na kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA vitakuwa na matoke mabaya kwa Marekani.
Maafisa waliotia saini taarifa hiyo wamesema kuwa, serikali ya Marekani haikutumia njia za kidiplomasia katika matakwa yake kwa Iran na kwamba Washington inaweza kufanya mazungumzo na Iran na nchi nyingine zilizotia saini makubaliano hayo juu ya jinsi ya kuyaboresha kwa kureje tena katika mkataba wa JCPOA.
Rais Donald Trump wa Marekani tarehe 8 Mei mwaka huu wa 2018 alikariri madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran na akatangaza kujiondoa nchi hiyo katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Nchi nyingine zilizotia saini makubaliano ya nyuklia na Iran ni Uingereza, Russia, China, Ufaransa na Ujerumani.