Oct 16, 2018 15:40 UTC
  • Picha ya

Picha ya "Mpalestina Mlemavu Katika Maandamano Makubwa ya Kurejea" imeshinda tuzo ya Bayeux Calvados-Normandy kwa waandishi wa habari za vita.

Tuzo ya Bayeux Calvados-Normandy ya Ufaransa hutolewa kila mwaka kwa waandishi wa habari na wapiga picha za matukio ya vita.

Picha hiyo ya Mpalestina Mlemavu Katika Maandamano Makubwa ya Kurejea imepigwa na Mahmud Hams, mpiga picha wa shirika la habari la AFP ikimuonyesha Saber Al-Ashkar, kijana mlemavu wa miguu wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 29, akiwa juu ya kiti cha magurudumu mawili huku anashiriki kwenye Maandamano Makubwa ya Haki ya Kurejea tarehe 11 Mei mwaka huu kwenye mpaka wa Ukanda wa Gaza, Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Maelezo ya picha hiyo yanasema: "Mpalestina Saber Al-Ashkar mwenye umri wa miaka 29, anarusha mawe wakati wa kukabiliana na askari wa Israel kwenye mpaka wa Ukanda wa Gaza, mashariki mwa mji wa Gaza, Mei 11, 2018 wakati Wapalestina wanaandamana kupigania haki ya kurejea kwenye ardhi yao ya kihistoria ambayo sasa ni Israel"

Saber Al-Ashkar, kijana mlemavu wa Kipalestina akishiriki kwenye Maandamano Makubwa ya Haki ya Kurejea

Thomas Coex, mkuu wa wapiga picha wa shirika la habari la AFP amesema: "Picha hii imepigwa katika mazingira magumu na hatari mno. Mpiga picha alikuwa katika maeneo ambayo hakuwa akipata msaada wowote, na hili ni jambo lenye thamani kubwa."

Tangu tarehe 30 Machi mwaka huu hadi sasa, Wapalestina wa Ukanda wa Gaza wameanzisha maandamano ya amani kwa anuani ya "Haki ya Kurejea" wakitaka kuhitimishwa kukaliwa kwa mabavu ardhi zao na kuondolewa mzingiro liliowekewa eneo hilo.

Wapalestina hao aidha wanataka litekelezwe azimio nambari 194 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo limezungumzia haki ya wakimbizi Wapalestina kurejea kwenye ardhi zao za asili.

Tangu yalipoanza maandamano hayo yanayoendelea hadi sasa,  Wapalestina zaidi ya 200 wameshauwa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa Kizayuni na wengine wapatao 22,000 wamejeruhiwa.../

Tags