Mar 16, 2024 11:16 UTC
  • Watoto wa Gaza; wahanga wakuu wa jinai za utawala wa Kizayuni

Kuchapishwa picha za vifo vya kutisha vya watoto wa Ukanda wa Gaza kutokana na njaa kwa mara nyingine tena kumepelekea kupuuziliwa mbali madai ya haki za binadamu yanayotolewa na nchi za Magharibi.

Siku 160 zimepita tangu utawala haramu wa Kizayuni uanzishe mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza. Wapalestina karibu elfu 32 wameuawa shahidi kufuatia jinai hizi tajwa za utawala wa Kizayuni. Watoto wa Gaza ni wahanga wakubwa wa jinai za utawala huo ghasibu unaoikalia Quds Tukufu kwa mabavu. Utawala wa Kizayuni si tu unawaua shahidi raia wa Kipalestina khususan watoto wadogo kupitia mashambulizi yake ya anga na nchi kavu; bali pia unatekeleza sera ya kuwasababishia njaa raia hao madhulumu wa Ukanda wa Gaza. Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa watu 4 kati ya 5 wanaokabiliwa na njaa kubwa duniani hii leo wanapatikana katika Ukanda wa Gaza. Ayman al-Safadi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jordan alisema katika hotuba yake juzi Alhamisi kuwa utawala wa Kizayuni unatumia chakula na dawa kama silaha dhidi ya Wapalestina katika hatua zake zinazokinzana na sheria za kimataifa. 

Ayman al Safadi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jordan 

Njaa imesababisha vifo vya kuhuzunisha vya watoto waliodhoofika na kukondeana kwa kukosa chakula. Katika siku za karibuni imechapishwa picha ya "Yazan al-Kaffarna", mtoto wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 9, ambaye alidhoofika sana na kuwa mifupa kutokana na utapiamlo kufuatia vita vinavyoendelea Ukanda wa Gaza. Mtoto huyo ameaga dunia baada ya kulazwa hospitalini kwa siku kadhaa.   

Shahidi, Yazan al-Kaffarna

Hali ya watoto wa Ukanda wa Gaza imekuwa mbaya zaidi na kulipelekea Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) kutoa wito wa kutolewa misaada ya chakula na kusisitiza kuwa watoto wa Kipalestina wanakabiliwa na baa la njaa na ufukara. Shirika hilo limeeleza kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watoto wa Kipalestina wanasumbuliwa na utapiamlo mkali. 

Hii ni katika hali ambayo njaa na utapiamlo mkali umesababisha kuenea kwa magonjwa miongoni mwa watoto huko Ukanda wa Gaza. Ripoti ya shirika la UNICEF imeeleza kuwa hivi sasa karibu asilimia 90 ya watoto walio na umri wa chini ya miaka 5 huko Gaza wanakabiliwa na moja ya magonjwa ya kuambukiza. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya UNICEF, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mpango wa Chakula Duniani (WFP). Mike Rayan Afisa wa WHO anayehusika na Hali za Dharura amesisitiza kuwa watoto wenye njaa na waliodhoofika walioathiriwa na mshtuko mkali wa kiakili wana uwezekano mkubwa wa kupatwa na magonjwa mnbalimbali. Shirika la Kuhudumia Watoto la UN limetangaza kuwa: "Vifo vya watoto ambavyo tulihofia kuwa vitatokea Ukanda wa Gaza sasa imekuwa kweli."  

Nukta muhimu hapa ni hii kuwa vifo vya watoto vinavyosababishwa na njaa na mashambulizi ya mabomu huko Gaza vinatokea mbele ya macho ya walimwengu. Hii ni katika hali ambayo maandamano  dhidi ya jinai za Wazayuni yanaendelea kushuhudiwa katika nchi mbalimbali duniani hata hivyo Umoja wa Mataifa umeshindwa kusitisha jinai hizo za Wazayuni. Uungaji mkono wa madola ya Magharibi hususan Marekani ndio sababu kuu ya Umoja wa Mataifa kushindwa kusimamisha jinai za Wazayuni.

Watoto wa Gaza wanataabika na njaa na maradhi mbalimbali 

Suala jingine muhimu ni kuwa viongozi wa Kizayuni wanaunga mkono rasmi na waziwazi jinai dhidi ya raia na hasa watoto wa Ukanda wa Gaza. Kuhusiana na hilo, Itmar Bin Gvir Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni alifika katika ofisi ya ukaguzi ya polisi wa utawala huo kwa ajili ya kuwaunga mkono askari polisi ambao Jumatano iliyopita walimuua shahidi kwa kumpiga risasi Rami Hamdan al Halhouli kijana Mpalestina aliyekuwa na miaka 12 katika kambi ya wakimbizi ya Shuafat huko kaskazini mwa Quds inayokaliwa kwa mabavu. Tovuti ya  Kiebrania ya "Waynet" imeinukuu ofisi ya Ben Gvir na kuandika: Msimamo wa waziri ni kwamba polisi wanapaswa kupewa tuzo na si kusailiwa na kuchunguzwa."

 

Tags