Dec 20, 2021 10:03 UTC
  • 2021; mwaka wa vifo vingi zaidi vya watoto wa Palestina katika kipindi cha miaka 7 iliyopita

Tovuti moja ya habari ya utawala wa Kizayuni wa Israel imeripoti kuwa, baada ya mwaka 2014 yaani wakati vilipotokea vita vya siku 51 na kuuawa shahidi idadi kubwa ya watoto wa Palestina, mwaka huu wa 2021 ndio ulioshuhudia idadi kubwa zaidi ya watoto wa Kipalestina waliouliwa shahidi na Israel.

Mapigano yanayotokea baina ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni husababisha vifo vya watu wengi wasio na hatia hasa wanawake na watoto wadogo. Watoto wa Kipalestina wanauliwa shahidi bure bilashi, hata kama hawashiriki kivyovyote vile katika mapigano hayo. Lakini pia watoto hao wanajeruhiwa, wanafanywa wakimbizi na haki zao zinakanyagwa kila leo na utawala katili wa Israel. Tab'an maisha ya tabu na majonzi wanayoishi watoto hao kutokana na kupoteza wazazi wao katika mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni ni janga jingine linalowatesa watoto wa Palestina katika umri wao wote. 

Khaled Quzmar, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kulinda Haki za Watoto wa Palestina amesema katika taarifa rasmi iliyoripotiwa na tovuti hiyo ya Israel kwamba tangu mwaka 2000 hadi hivi sasa, watoto 2000 wa Palestina wameuliwa shahidi na wanajeshi makatili wa utawala wa Kizayuni na hiyo ni idadi kubwa zaidi ya Wapalestina waliowahi kuuliwa shahidi na Wazayuni katika kipindi cha mwaka mmoja tangu 2014. Ripoti hiyo inaongeza kuwa, mwaka huu wa 2021, watoto 86 wa Palestina wameuawa shahidi katika jinai za wanajeshi Wazayuni na walowezi wa utawala wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Ghaza. 

Wasaliti wa kadhia ya Palestina

 

Kwa kweli kuna sababu tofauti zinazopelekea kuwa mbaya sana hali ya watoto wadogo wa Palestina hasa katika mwaka huu wa 2021.

Moja ya sababu hizo ni vita vya siku 12 vilivyotokea kwenye Ukanda wa Ghaza. Vita hivyo vimekuwa na madhara makubwa na miongoni mwake ni maafa ya kibinadamu. Wapalestina 256 waliuawa shahidi katika kipindi cha siku 12 tu za vita hivyo huku 66 kati yao wakiwa ni watoto wadogo. Hii ina maana kwamba kati ya kila Wapalestina wanne waliouliwa shahidi na wanajeshi makatili wa Israel kwenye vita hivyo vya siku 12, mmoja wao alikuwa mtoto mdogo. Watoto wengine 6000 wa Kipalestina walijeruhiwa katika vita hivyo, suala ambalo linazidi kuthibitisha kwamba wahanga wakuu wa vita hivyo walikuwa ni watoto wa Palestina. 

Sababu nyingine ni kuendelea kuzingirwa kila upande Ukanda wa Ghaza. Wakazi wa ukanda huo ambao wanakadiriwa kupindukia milioni mbili, wamefungiwa njia zote za kuingia na kutoka, za ardhini, angani na baharini na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa miaka 15 sasa na wanaishi katika mazingira magumu sana ya kiuchumi. Jinai hiyo ya Wazayuni inawasababishia maafa makubwa ya kibinadamu wananchi madhlumu wa Palestina ikiwa ni pamoja na kukaukiwa na chakula, madawa na vitu vingine muhimu na hiyo ni sababu ya kuuawa shahidi watoto wasio na hatia wa Palestina.

Khalid Mash'al

 

Jambo la kutia akilini hapa ni kwamba, mwaka 2021 umekuwa mwaka wa vifo vingi zaidi za watoto wa Palestina kwenye kipindi cha miaka 7 iliyopita katika hali ambayo, mwezi Septemba mwaka jana 2020, nchi za Kiarabu za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Bahrain zilitangaza rasmi uhusiano wao na utawala katili wa Israel. Nchi hizo zilidai kuwa eti kutangaza kwao uhusiano rasmi na Wazayuni ni kwa ajili ya amani na kulinda maslahi ya Wapalestina. Hata hivyo hali mbaya ya watoto wa Palestina mwaka 2021 inathibitisha kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umezidi kupanda kiburi cha kufanya ukatili mkubwa zaidi dhidi ya Wapalestina baada ya kupata uungaji mkono wa nchi hizo dhaifu za Kiarabu. Utawala wa Kizayuni unatambua vyema kuwa hakuna sauti yoyote itakayotoka kwenye nchi hizo za Kiarabu ya kulaani jinai za Israel. 

Hata hivyo, usaliti wa baadhi ya nchi za Kiarabu na kuongezeka jinai za Israel hakujalidhoofisha taifa la Palestina na ndio maana Khaled Mash'al, mkuu wa harakati ya HAMAS nje ya Palestina akaonya kwa kusema, sisi tunahisi kwamba tumekaribia mno kwenye sekunde nyeti sana ya mzozo baina yenu na Wazayuni. Vita baina yetu na wavamizi wa Quds havijabakia muda mrefu kumalizika na mlingano wa nguvu ni kwa manufaa ya taifa la Palestina.

Tags