Marekani yajitoa kimasomaso kwa kuwawekea vikwazo watu waliohusika kumuua Khashoggi
Wizara ya Hazina ya Marekani na katika hatua yake iliyochelewa, imewawekea vikwazo raia kadhaa wa Saudi Arabia kutokana na mauaji dhidi ya Jamal Khashoggi, mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa Aal-Saud.
Wizara ya Hazina ya Marekani imetangaza kuyaweka katika orodha nyeusi majina ya watu 17 raia wa Saudia kutokana na kushiriki kwao katika mauaji ya mwandishi huyo. Saoud Al Qahtani na Mohammad Al-Otaibi, balozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki ni miongoni mwa watu waliowekwa katika orodha nyeusi ya vikwazo vya Marekani. Hatua ya Wizara ya Hazina ya Marekani, imetajwa na weledi wa mambo kuwa ni aina ya kujisafisha Washington kuhusiana na faili hilo. Hii ni katika hali ambayo awali rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa, nchi yake haitokata mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia kutokana na mauaji ya Khashoggi.
Hii ni katika hali ambayo kundi moja la maseneta nchini Marekani limetaka kufuatiliwa faili la mauaji ya mwandishi huyo, suala ambalo hata hivyo halikufanywa na ikulu ya nchi hiyo (White House). Jamal Khashoggi alitoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya kuingia katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, tarehe Pili Oktoba. Awali utawala wa kifalme wa Saudia ulikadhibisha kuhusika kwa namna yoyote na mauaji au kupotea kwa Khashoggi, hata hivyo na kutokana na mashinikizo ya walimwengu tarehe 18 ya mwezi huo ukalazimika kukubali na kudai kwamba mwandishi huyo alipotea maisha katika vurugu zilizoibuka kati yake na mfanyakazi mmoja wa ubalozi huo.