Nov 16, 2018 16:41 UTC
  • Mynamar yawakamata Warohingya 106 wakielekea Malaysia

Maafisa wa Idara ya Uhamiaji wa Myanmar wamewatia nguvuni Waislamu 106 wa Rohingya ambao walikuwa safarini kuelekea Malaysia.

Kyaw Htay, ofisa wa idara hiyo amesema Warohingya hao wamekamatwa mapema leo nje kidogo ya mji wa Sittwe, umbali wa kilomita 30 kusini mwa eneo la Yangon baada ya boti yao kuharibika wakiwa safarini kuelekea nchini Malaysia.

Waislamu hao wa Rohingya walikuwa wakiishi katika kambi za wakimbizi katika mji wa Sittwe, makao makuu ya mkoa wa Rakhine. 

Hii ni katika hali ambayo, ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na Mpango wa Ujenzi wa umoja huo ilisisitiza kuwa Waislamu Warohingya wangali wanaishi kwa hofu na hawana imani yoyote kuhusu usalama wao. Ripoti hiyo imeongeza kuwa, Waislamu hao hawana hata ruhusa ya kutembea kwa uhuru katika eneo wanaloishi la mkoa wa Rakhine. 

Warohingya wanaishi kama wakimbizi ndani ya nchi yao

Jumanne iliyopita, Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa aliitaka serikali ya Bangladesh kusimamisha mpango wake wa kuwarejesha kwa nguvu nchini Myanmar maelfu ya wakimbizi Waislamu wa Rohingya akisisitiza kuwa, maisha yao yatakuwa hatarini na kwamba mazingira ya kuwapokea hayajaandaliwa.

Kwa mujibu wa UN, malaki ya wakimbizi Waislamu wa Rohingya wamekimbilia nchini Bangladesh, India na Malaysia tangu Agosti mwaka jana 2017, baada ya wanajeshi wa Myanmar wakishirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali kuanzisha wimbi jipya la mauaji na hujuma dhidi ya Warohingya katika mkoa wa Rakhine nchini Myanmar.  

Tags